Joseph Lyimo,Arumeru
MGOGORO mkubwa unafukuta baina ya wakazi wa
kitongoji cha Msikitini Kijiji cha Mikungani wilayani Arumeru na Mwenyekiti wa
Kitongoji hicho wakimtuhumu kuruhusu kituo cha kulea watoto yatima kujengwa
kwenye barabara wanayoitumia hivyo kuwa kikwazo cha maendeleo.
Wakizungumza jana kwenye kikao kilichoitishwa
na Ofisa Tarafa wa Mbuguni Japhet Moirana wakazi hao walisema hawapingi
maendeleo ya kituo hicho ila wanapinga uongozi wa kitongoji kuruhusu ujenzi huo
na kufunga barabara yao.
Mmoja kati ya wakazi hao Hamad Ngoya alisema
uongozi wa kitongoji hicho ulifanya makosa kuruhusu ujenzi wa kituo hicho
kwenye barabara inayotumika tangu mwaka 1975 hivyo jengo hilo limejengwa hivi
karibuni kwa makosa.
“Barabara ni maendeleo kwani hata nyumba ya
mama wa Rais Jakaya Kikwete iliyopo Msoga Bagamoyo ilijengwa barabarani na
akaruhusu ibomolewe na Tanroads hivyo siyo busara kujenga kituo hicho barabarani,”
alisema Ngoya.
Naye,Lewis Msaiyo alisema hata kama kituo
hicho kinataka kuziba barabara kwa sababu ya usalama wa watoto kugongwa na gari
au pikipiki wangepaswa waweke matuta au ukuta kuliko kuziba barabara hiyo
inayosaidia watu wengi.
Kwa upande wake,Tareto Dau alidai kuwa
barabara hiyo ilitolewa bure mwaka 1975 na Mzee Tareto na Bakary Ngoya ili
jamii ipite kwenye njia hiyo na kufuata huduma mbalimbali ikiwemo kununua
bidhaa kwa duka la Fakhii na Ally Mnaro.
Zawadi Amiry alisema uongozi wa kituo hicho
haukupanga mipango yake kwa ukamilifu kwani endapo wangetambua kuwa eneo la
ekari moja walilonalo ni dogo wangejenga ghorofa kuliko kujenga kituo chao
pembeni ya barabara.
Hata hivyo,Kiongozi wa kituo hicho Mchungaji
Frank Lema alisema yeye hana ugomvi na mtu yeyote ila uamuzi wowote
utakaochukuliwa na wakazi hao wenyewe wataukubali kwani awali walielezwa kuwa
barabara hiyo haitumiki.
Naye,Ofisa Tarafa wa Mbuguni Japhet Moirana
alisema sakata hilo linarudishwa kwenye mkutano mkuu kijiji cha Mikungani ndiyo
wenye uamuzi wa mwisho na kudai kuwa awali alielezwa Serikali ya kijiji
imekubali ujenzi huo eneo hilo.
Moirana alisema barabara hiyo iendelee
kutumiwa na jamii hadi hapo itakapoamriwa vinginevyo na pia aliiasa jamii hiyo
ikubali barababara hiyo iondolewe eneo hilo wazo lililopingwa vikali na wakazi
hao.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment