Thursday, October 11, 2012

Halmashauri ya wilaya ya Karatu iliyoko mkoani Arusha imeamua kumbadilishia mazingira ya kazi mwalimu wa shule msingi ya Barakta kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuiba mali ya shule zinazomkabili.


Na Bertha Ismail,karatu

Halmashauri ya wilaya ya Karatu imefikia hatua hiyo baada ya wazazi wa wanafunzi kugoma watoto wao kuhudhuria shule kwa muda wa siku tatu mfululizo kushinikiza kumkataa mwalimu huyo aliyejulika kama Anjelina Sarwat kutokana na tabia hiyo ya kuiba mara kwa mara mali ya shule ikiwemo chakula kilichotolewa msaada na mpango wa chakula duniani (WFP).

Wakiongea kwenye mkutano mkuu wa kata, ikiwa ni siku ya tatu ya mgomo wao wananchi hao walisema kuwa wamechoshwa na tabia ya mwalimu huyo ya kuiba mara kwa mara mali ya shule kwa kujinufaisha yeye na familia yake ambapo pia wamemtuhumu vikali mwalimu huyo kujihusisha na maswala ya kishirikina.

Aidha kikao hicho pia kimetokana na vilio na majonzi ya hofu iliyotanda usiku wa septemba 28 baada ya kumkamata mtoto wa mwalimu huyo (Paskali Raphael) katika vyanzo vya maji (mto na kisima) akinyunyizia dawa  kwenye maji iliyoshirikishwa na imani za kishirikana hali iliyoamsha hisia za watu hao na kuamua kupiga yowe usiku huo.

Hata hivyo baada ya kilio hicho viongozi wa serikali walifika eneo la tukio na kukuta dawa hizo zilizowekwa pembezoni mwa kisima cha maji ambayo ni tegemezi pekee kijijini hapo na kuamua kuwatuliza wananchi na kumkamata kijana huyo kwa mahojiano ya awali ambapo alisema kuwa alichukua dawa hizo kwa ajili ya kuwatuliza wananchi na uhasama waliyonayo dhidi ya familia yao.

Akiongea na waandishi wa habari diwani wa kata ya Kansay John Pissa alisema kuwa chanzo cha wazazi hao kugomea watoto wao wasiudhurie shule ni baada ya kuchoshwa na tabia ya mwalimu huyo ya kukamatwa kwa nyakati tofauti na mali za shule na pindi akiulizwa hudai kurejesha ikiwemo gunia la mahindi, gunia la maharage pia ndoo ya mafuta pamoja na mabati matano ya shule hiyo ya Barakta.

Hata hivyo baada ya mgomo huo Halmashauri ya wilaya ya Karatu imeamua kumuamisha mwalimu huyo kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo na kumpeleka katika shule ya msingi Ayalaliyo iliyoko wilayani hiyo hiyo ya Karatu.

Afisa elimu shule za msingi Bwana Kinyemi M. Sepetu alisema kuwa ingawa mwalimu huyo alikiri kukutwa na mabati hayo lakini alikana kuwa ni mali ya shule na kuomba halmashauri imlinde ndipo kuamua kumuhamishia shule ya Ayalaliyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Hata hivyo uamuzi huo wa halmashauri kumuhamisha mwalimu huyo bila kumpa adhabu yoyote kwa kuiba mali ya umma imezua minong’ono na kuona mwalimu huyo anatetewa na halmashauri hali itakayowafanya walimu wengine kueneleza tabia hiyo kwa adhabu ya kuamishwa.

No comments:

Post a Comment