WAZIRI MKUU ATAKA WAJASIRIAMALI WAWE MAKINI
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifurahia moja kati ya viatu
vilivyoonyeshwa kwenye banda la Mareshi Shoe Maker katika kilele cha
sherehe za kutoa ruzuku kwa wajasiliamali waliofanya vizuri katika
Progamu ya fanikiwa kibiashara zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi
mmoja jijini Dar es salaam Juni 30,2012.Kulia kwake ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwezeshaji na Uwekezaji, Dkt,
Mary Nagu na kulia Mwenyekiti wawa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania,
Mama Ester Mkwizu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka
wajasiriamali wa kati na wadogo nchini wawe waangalifu na makini katika
biashara wanazopanga kuzifanya kama kweli wanataka kufanikiwa maishani na
akawaonya wale waliopata mbegu mtaji kuchukua tahadhari zaidi.
Ametoa onyo hilo leo mchana
(Jumamosi, Juni 30, 2012) wakati akizungumza na wajasiriamali kutoka mikoa yote
ya Tanzania Bara na Visiwani ambao walihudhuria sherehe za kutoa zawadi kwa
washiriki wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (Business Development Gateway - BDG)
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Naomba
niwatahadharishe kuwa ujasiriamali unataka umakini wa hali ya juu. Mmoja wa
Wajasiriamali mashuhuri huko Marekani aliwahi kutoa tahadhari kwa kusema: "Business is like oil, it won't mix
with anything but Business" akimaanisha kwamba biashara ni kama mafuta
ya kulainisha mitambo (oil) ambayo
hayachanganywi na kitu kingine chochote, isipokuwa oil yenyewe. Tunahitaji uangalifu na umakini katika kufanya biashara
zetu bila kuchanganya na mambo mengine
Amesema mtu anapochukua mkopo kwa nia
ya kuanzisha biashara kisha akaamua kuoa mke wa tatu au kununua gari kwa
kutumia fedha hiyo ya mtaji ni lazima atakwama kwa sababu atakuwa amechakachua
dhima nzima ya ile biashara yake.
Alisema katika mabanda ya maonesho aliyotembelea
leo, ameona changamoto kuu tatu ambazo zinahitaji kuangaliwa haraka ili kuinua
soko la bidhaa za wajasiriamali hao.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni
ukosefu wa vifungashio bora, ukosefu wa alama za viwango kutoka shirika la
viwango nchini (TBS) na ukosefu wa alama ya biashara (bar code) katika bidhaa
zao. “Bidhaa zenu ni lazima ziwe na vifungashio vizuri vyenye mvuto ili mnunuzi
ashawishike kununua.”
“Nawasihi mfuate masharti ya shirika
la viwango nchini ili bidhaa zenu zikubalike, waoneni wahusika ili mpate bar code kwenye bidhaa zenu. Bidhaa zenu
zikiwa na bar code zitakubalika
kokote ulimwenguni,” alisisitiza.
Waziri Mkuu pia alisema anatatizwa na
changamoto moja kuu ambayo ni ya kuhakikisha mpango wa BDG unaendelezwa ili
uwanufaishe watu wengi zaidi. “Mpango huu umefikia mwisho, na umedumu kwa miaka
minne tu. Mwenyekiti wa TPSF itabidi tuangalie hata uwezekano wa kukopa ili
jambo hili zuri lisiishie hapa,” alisema.
No comments:
Post a Comment