Wanakijiji wailalamikia Serikali Kuu
WANAKIJIJI wa kijiji cha Mkambarani Morogoro Vijijini, wameilalamikia Serikali Kuu na halmashauri ya Wilaya kwa kumuingiza mwekezaji kutoka Korea katika kijiji jirani cha Pangawe na kutumia rasilimali maji bure bila kuwashirikisha.
Wananchi hao kutoka katika kijiji cha Mkambarani Kata ya Mkambarani wilaya ya Mororgoro vijiji na viongozi wao wa kata wameishutumu ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkoa na Wizara ya ardhi na maendeleo ya makazi kwa kuwaingiza wawekezaji wanaoendesha mradi wa kijiji cha mfano cha Pangawe bila kuushirikisha uongozi wa kata na kuanza kutumia maji ya kijiji cha Mkambarani ambao hawakuuchangia.
Tarafa ya Mikese yenye kata 3 na vijiji 11 haina maji safi ya kunywa isipokuwa kijiji cha Mkamabarani ambacho kimekuwa na mradi wake unaotegemewa na vijiji vingine, lakini mradi huo umeteka maji hayo wakati wananchi wanazuiwa kufunga bomba nyumbani kwao.
Wakizungumza katika mrejesho wa utafiti raghibishi wa kijamii (PAR) uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika kata hiyo, wakati wa mrejesho ngazi ya wilaya, wananchi hao na Viongozi wa kata wamesema kuwa mradi wa kijiji cha mfano kwa ushirikiano na Korea Kusini hawakushirikishwa.
Pamoja nayo wamesema kuwa kata hiyo inachangamoto nyingi ambazo zinasababishwa na uongozi mbovu licha ya wananchi wake kujitahidi kuibua na kuchangia miradi mbailimbali.
Katika utafiti huo, changamoto lingine imeonesha wananchi wa Mkambarani hawana ardhi ya kulima mazao ya chakula kutokana na ardhi waliokuwa wakitumia kuchukuliwa na mwekezaji huo na kufye mahindi ya wananchi kitendo kilichosababisha mgogoro kati yao na mgeni huyo.
Akizungumzia mradi huo, Mtandaji wa kata ya Mkambarani, Msekwakadodo Makoko, amesema kuwa uongozi wa kata haikushirikishwa kwenye mradi huo walishangaa wageni wanafika katika kijiji kuuzindua.
“sisi tulishangaa kuona Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Pangawe wamepanda ndege kwenda Korea Kusini, waliporudi Waziri Mkuu akaja kuufungua mradi, sisi Kata hatujui chochote, kwa kweli sisi tunausikia tu hatujui ni utaalam gani anaoutoa huyo Mwekezaji,” ameeleza Makoko.
Amesema pia kuwa wanachosikitika ni kwamba maji ambayo wananchi wa Mkambarani walichangia asilimia 5 sasa yanaenda kwa mwekezaji huyo huku wananchi wakikatazwa kuyatumia.
Afisa Kilimo Wilaya ya Morogoro Joseph Malaki amesema kuwa mradi huo wa Korea na Tanzania unalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kitaalam kama mafunzo, lakini akalalamikia sera za nchi ambazo zinakubali misaada yenye masharti magumu. “sera za nchi ndo zinazoelekeza ujio wa wageni pamoja na masharati yao, wanakuja na wanasema wanafanya na wataalam wao hatina jinsi, huu ni udhaifu wa sera zetu…,” amesema Ofisa Kilimo huyo.
Akitoa mrejesho wa utafiti huo, mtafiti kutoka TGNP Dinah Nkya amesema kuwa Utafiti umegudua changamoto nyingi ambazo zinaikabili jamii ya kijiji hicho, ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na serikali ngazi zote.
Masuala makuu ambayo yameibuliwa na jamii katika kijiji hicho ni ukosefu wa maji ya kutosha katika kijiji hicho, wanakijiji wa Fulwe kukosa kabisa maji ya kutumia na kulazimika kununua maji kwa sh. 500 kwa lita 20. Suala lingine ni mgogoro wa ardhi unaotokana na ardhi ya wananchi kuchukuliwa na mwekezaji na taasisi za kiserikali na kidini.
Changamoto nyingine ni kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa wasichana wanaofanya kibarua katika mradi huo wa Korea ambapo wanakijiji waliutaka uongozi wa wilaya kumfuatilia mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi kwenye mradi huo ambaye amekuwa akiwadhalilisha wasichana kijinsia.
Kutokana na hilo, mwanchama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (MVIWATA) Mkoa wa Morogoro, Maricelina aliwataka wananchi kuchukua hatua za haraka kudhibiti tatizo hilo ikiwepo kushinikiza uwajibikaji wa viongozi wa ngazi ya kijiji, kata na wilaya.
“Tusipochukua hatua za haraka tutaharibu jamii yetu na hasa vijana wa kesho, wananchi tushikamane, tupambane na watu wanaokuja kutuharibu na kutudhalilisha kijinsia, kwanini asioe anaharibu watu kimaumbile?….,” alisema.
Pia tatizo la mimba za utotoni limeibuliwa kuwa ni tatizo kubwa katika kata hizo kutokana na kukosekana kwa mabweni katika shule ya sekondari Nelson Mandela, ili kuwapa wasichana ulinzi wa kutosha na kuacha kuishi kwenye nyumba za kupanga mitaani.
Aidha changamoto nyingine iliyoibuliwa ni kukosekana kwa soko la kuuzia bidhaa zao za mazao. Wananchi wameitaka serikali kumtaka mwekezaji kampuni ya Mkonge kurudisha sehemu ya shamba kijijini ili litumike sehemu ya soko katika kata hiyo.
*Imeandaliwa na Programu ya Habari na Mawasiliano TGNP
No comments:
Post a Comment