Wednesday, June 20, 2012

Binti asimulia mamaye alivyouawa kinyama

Binti asimulia mamaye alivyouawa kinyama


Ni ukatili usioelezeka, ni kukosa hata chembe ya ubinadamu, hii ni simulizi ya kutisha ya binti aliyeshuhudia mama yake akicharangwa mapanga kutokana na imani za kishirikina.
Hakuna uchungu zaidi duniani ambao mwanadamu huupata pale anapofiwa na mmoja wa wazazi wake awe mama ama baba.
Uchungu huu huupata bila kujali kuwa kifo hicho kimesababishwa ama na maradhi au na umri kufikia kikomo na hivyo kwa vyovyote vile kama binadamu anapaswa kuondoka duniani kama mola alivyopanga.
Hakika, kufiwa na mzazi ni kama mwisho wa yote na kama kungekuwa na uwezekano, kila mmoja angependa wazazi wake waendelee kuishi milele!
Kama hivi ndivyo, hebu fikiria msichana huyu, Tatu Michael (19), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lwenzira, iliyopo Wilaya ya Geita mkoa mpya wa Geita, aliyeshuhudia mama yake mzazi, Esther Konya (55), akiuawa kikatili na kundi la watu kwa kucharangwa mapanga kutokana na imani potofu za kishirikina yu katika hali gani ya majonzi na ameathirikaje kisaikolojia.
Mama wa mwanafunzi huyo, ni mmoja wa wanawake vikongwe wanne waliouawa kwa mpigo Mei 10, mwaka huu katika kitongoji cha Chenzumla kijiji cha Lwenzera wilayani Geita kutokana na imani za kishirikina.
Mkoa mpya wa Geita, ni miongoni mwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo jamii yake imejenga imani kubwa kwamba kila kifo ama ugonjwa unapotokea katika familia zao, husababishwa na mkono wa mtu kwa maana kurogwa! Mikoa ambayo mauaji ya namna hii yamekithiri ni Shinyanga na Mwanza.
Vikongwe wengine waliouawa pamoja na Konya kutokana na imani hizo na nyumba pamoja na mali zao zote kuteketezwa kwa moto ni Lolensia Bangili (70), Kulwa Mashana (65) na Roza Masebu (65).
Chanzo cha mauaji hayo ya kikatili ni mtoto Diana Salu (5), kuuawa na kuliwa fisi, tukio ambalo wanakijiji walilihusisha na imani za kishirikina ya kwamba mnyama huyo alikuwa amefugwa kimazingara na mmoja wa vikongwe hao.
Baada ya mtoto Dina kuuawa na fisi huyo Mei 9, mwaka huu, saa 1:30 usiku, ndipo wanakijiji walipopiga yowe maarufu kama `mwano’ kwa lugha ya Kisukuma na kuanza kumsaka fisi huyo mla watu.
Hata hivyo, walipomfurumusha fisi huyo katika vichaka vya kijijini hapo, aliwapotea jirani na nyumba ya mmoja wa vikongwe hao, jambo lililowafanya wanakijiji waamini kuwa ameingia ndani ya nyumba ya kikongwe na hivyo wakaanza kumshambulia bibi huyo kwa mapanga na shoka hadi walipomuua.
Wanakijiji hao hawakuishia hapo, walikwenda katika nyumba ya kila kikongwe moja baada ya nyingine na kufanya mauaji hayo pamoja na kuteketeza nyumba zao kwa moto.
Msichana Tatu, alikuwa ni shuhuda wa mama yake akicharangwa mapanga kikatili hadi alipokata roho kama anavyosimulia mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyetembelea kijiji hicho hivi karibuni.
“Siku moja kabla ya tukio la kuuawa kwa mama yangu majira ya saa moja jioni, nilikuwa nauza uji katika kijiwe chetu cha Lwenzira.
Nilikuwa nikifanya biashara hiyo kwa lengo la kutafuta fedha za ada ya mtihani wa taifa na mwisho wa kuwasilisha tulielezwa kwamba ni Mei 21, mwaka huu,” ndivyo alianza kusimulia msichana Tatu, ambaye wazazi wake walitengana miaka kadhaa iliyopita hivyo yeye akabaki chini ya uangalizi wa mama yake.
Anasema wakati akiendelea na biashara yake, alifika kijiweni hapo mtoto Dina Salu, akanunua karanga na kuondoka kuelekea nyumbani kwao maeneo ya kijijini hapo.
Hata hivyo, anasema baada ya dakika chache, alitokea kijana mmoja akiendesha pikipiki na kuwaeleza waliokuwa wakifanya biashara pale kijiweni kwamba yule mtoto (Dina), amebebwa na fisi.
Anasema punde si punde ulipigwa `mwano’ (yowe) ambapo wanakijiji walikusanyika mara moja na kutangaziwa mkasa huo, hivyo walianza mara moja kumfuatilia fisi huyo vichakani lakini aliwapotea.
“Nami niliamua kukusanya vifaa vyangu vya biashara na kuondoka haraka kuelekea nyumbani. Nilipofika mama alinihoji kelele zinazopigwa pale kijijini zilihusu nini, nami nilimsimulia kuwa kuna mtoto amechukuliwa na fisi,” anaeleza Tatu.
Anaongeza: “Mwano huo uliendelea hadi alfajiri ya siku iliyofuata (Mei 10, mwaka huu), na baadaye zilitolewa taarifa kwamba mabaki ya mtoto Dina, yameonekana vichakani huku mguu na sehemu zake za siri zikiwa zimetafunwa.
Anasema baada ya hapo, kuna kundi la watu lililobaki pale kwenye mwili wa mtoto na kundi lingine hususan vijana, lilianza kuzunguka kijijini kwenye nyumba za vikongwe ambao wamekuwa wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
“Muda si mrefu, kundi hilo lilifika katika nyumba yetu na mmoja wao alisema `ndiyo hapa kwa `mkukulu’, yaani kikongwe na hivyo kundi hilo la vijana takriban mia mbili, likasimama,” anasema na kufafanua kuwa wakati huo mama yake, alikuwa ni mmoja wa waliobaki eneo uliopo mwili wa mtoto aliyeliwa na fisi.
“Niliwauliza watu hao kwanini wanasema hapa hapa kwani kuna nini, ambapo nilijibiwa kwa jazba na mmoja wao kuwa niache upumbavu na uchawi wetu,” anafafanua.
Kwa mujibu wa Tatu, watu hao ambao baadhi aliwafahamu kwa sura, kila mmoja alikuwa amebeba silaha yake yakiwemo mapanga, shoka, marungu, fimbo na wengine majembe.
Tatu anasema mmoja kati ya watu hao, alikuwemo kijana mmoja ambaye aliwahi kumtaka kimapenzi, lakini alimtolea nje kwa kuwa malengo yake ni kusoma.
“Mara nikasikia, lete nyasi na kibiriti tuwashe moto nyumba yake. Muda si muda, nikaona moja ya pembe ya nyumba yetu inawaka moto na kona nyingine pia zikafuatia,” anasema.
Anaongeza: Kwa ujasiri mkubwa, nilikimbilia ndani kuchukua begi langu la nguo lakini yule aliyewahi kunitaka kimapenzi, alinikimbiza na kuninyang’anya kisha akalitupia ndani ya nyumba iliyokuwa ikiteketea kwa moto huku akisema ujanja wangu leo umefikia kikomo.”
Ndani ya begi, Tatu anasema kulikuwa pia na Sh. 58,000 alizokuwa amezikusanya kutokana na biashara yake ya uji kwa ajili ya ada ya mtihani wake wa kidato cha nne na Sh. 100,000 za mama yake alizopewa na binti yake mkubwa, Felister Michael, kwa ajili ya matumizi.
“Nikakumbuka tena kuwa ndani ya nyumba yetu iliyokuwa ikiteketezwa kwa moto, kulikuwa na sare zangu za shule na madaftari. Hivyo niliamua kujitosa ndani na kwenda kuvichukua, lakini watu wale wasiokuwa na huruma, walininyang’anya na kivirushia ndani ya moto!,” anasema kwa masikitiko makubwa.
Anasema kitendo cha kumchomea madaftari yake kilimsononesha mno kwa kuwa atashindwa kujisomea yale aliyokuwa akifundishwa na walimu wake.
Kwa mujibu wa Tatu, mali na vyakula vyote vilivyokuwemo ndani ya nyumba yao, viliteketezwa kwa moto. Tatu anasema wakati akihaha kujaribu kuokoa madaftari, sare na fedha za ada na matumizi huku watu hao wakimnyang’anya na kuvitia ndani ya moto, baadhi ya akina mama wachache waliofika eneo la tukio, walimuonya kuwa akimbie pamoja na wadogo zake kwani kundi hilo la watu wenye hasira, lingehatarisha pia maisha yao.
“Niliwakusanya watoto watano na kwenda kujificha chini ya mwembe mita chache kutoka katika nyumba yetu na kuendelea kushuhudia ikiteketea kwa moto,” anasema.
Hata hivyo, anasema wakati yote hayo yakiendelea, mama yake aliyekuwa katika eneo ulipo mwili wa mtoto Dina, aliyeuawa na fisi, alifika katika nyumba yake akiwa ameshikilia kandambili mkononi na kukuta ikiteketea kwa moto huku kundi kubwa la watu likiwa limezingira eneo lake.
“Mama alianza kupiga yowe na kuwahoji watu hao sababu za kuchoma moto nyumba yake ambayo aliijenga kwa nguvu zake baada ya kutengana na mumewe. Alisema kwanini wanachoma nyumba yake ataiishi wapi na wanawe?,” anasema Tatu kwa huzuni.
Anasema alipotamka hivyo tu, baadhi ya watu katika kundi hilo walisema: “Kumbe ndiye huyu? Na bila kupoteza muda, walimvamia na kuanza kumcharaza mapanga, shoka na wengine wakimshambulia kwa fimbo.”
“Sitasahau katika maisha yangu yote siku ile maana niliona kwa macho yangu mama akicharangwa mapanga mithili ya mnyama.
Mmoja alikata mapanga katika miguu yake yote mpaka mifupa ikatokeza nje akadondoka chini na mwingine akamcharanga panga kichwani,” anasema Tatu kwa uchungu mkubwa huku akimwaga machozi na kumfanya dada yake, Felister Michael (27), naye abubujikwe machozi mfululizo.
Anaongeza: “Baada ya mama kuanguka chini, walimuona bado anahema, mmoja wa watu hao akasema kwa sauti ‘kumbe bado’, ndipo alipomcharanga panga katikati ya tumbo na mama akakata roho mimi nikishuhudia pamoja na wadogo zangu pale katika kichaka cha mwembe tulipojificha,” anasema na kuzidi kububujikwa machozi.
Itaendelea kesho
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment