Sunday, June 17, 2012

‘Ashindwa kujiunga na Sekondari Handeni kwa kukosa ada’



‘Ashindwa kujiunga na Sekondari Handeni kwa kukosa ada’

Mwanafunzi Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni akimuonesha mwandishi fomu ya kuitwa shuleni
Mama wa mtoto huyo, Hadija Magalu
Na Joachim Mushi, Handeni
LICHA ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na kidato cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule kutokana na kipato duni cha familia zao.
Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi walioshindwa kujiunga na sekondari kutokana na mama yake kushindwa kumgharamia mahitaji ya shule.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, wilayani Handeni, katika utafiti uliofanyika kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), mama wa mtoto huyo Hadija Magalu aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu alisema ameshindwa kumsomesha mwanaye kutokana na kipato duni alichonacho.

Mwenjuma M. Magalu (kulia) akiwa na Bibi yake nyumbani kwao Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni

Magalu alisema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu Desemba 12, 2011 na kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule ulipofika (Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.
“Naweza kukuonesha hata baadhi ya vitu ambayo nilikuwa tayari nimenunua kama sare, kwanja na mahitaji mengine madogo madogo…aliyenikwamisha na kunivunja moyo ni babayake (baba wa mtoto), ambaye awali niliwasiliana naye kupitia kwa ndugu zake na kuahidi angenisaidia ada lakini hakufanya hivyo hadi muda wa kwenda shule ulipofika,” alisema Magalu.

Mume wa Magalu (jina tunalo) ametelekeza familia yake (watoto wanne) pamoja na mkewe kwa zaidi ya miaka minne sasa kwa kisingizio kwamba amekwenda nje ya Wilaya ya Handeni kutafuta maisha, huku mkewe akibaki akiangaikia familia hiyo.
“Tumekuwa tukisikia tu kwamba ameonekana kijiji fulani lakini ukifuatilia humpati, na mara nyingi anapowasiliana na ndugu zake ndio wanatupa taarifa zake…nami niliwasiliana naye mara ya mwisho nikimpata taarifa za mtoto kufaulu lakini hakutekeleza ahadi yoyote juu ya kunisaidia ada ya mtoto.

Michango iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga na kidato cha kwanza ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha ya madawati 15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi sh. 5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh. 2,000.

Akihutubia Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania lililomalizika hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma na Tanga, wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Hata hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa moja ya kampuni za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha Msasa, kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.

Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake haina taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi amueleze mtoto huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na ikiwezekana kusaidiwa.

“Kama huyo mtoto yupo mwelekeze aje pale ofisini kuna wataalamu wa utambuzi watamuhoji na kuangalia namna ya kumsaidia…sisi hatuna taarifa hizo na huenda wahusika wanatuficha,” alisema kiongozi huyo.

No comments:

Post a Comment