Friday, November 3, 2017

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeunga mkono juhudi za Umoja wa Boda Boda Jiji la Arusha (UBOJA) za kutaka kuanza kusajili wanachama wake pamoja na vituo vyote kwa njia ya kisasa katika mfumo wa kompyuta kama hatua ya kuweka kumbukumbu itakayosaidia watambulike haraka kwa sura, majina yao, vyombo vyao vya usafiri na maeneo yao wanayoishi kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya.

Akizungumzia nia ya kufanya hivyo na namna itakavyotekelezwa jana katika ukumbi wa bwalo la Polisi ulilopo jijini hapa, Mwenyekiti wa UBOJA Bw. Maulid Makongoro alisema kwamba wameamua kufanya hivyo ikiwa ni mkakati wa kuliunga Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu.

Bw. Makongoro alieleza ili kufanikisha suala hilo la usajili, kila kituo kitatakiwa kwanza kilipe ada ya mwaka mzima lakini pia kitatakiwa kulipia gharama ya Shilingi 20,000 ambapo wanachama wake bila kujali idadi waliyonayo wote watapigwa picha na taarifa zao zitapelekwa kwa viongozi wa wilaya likiwemo Jeshi la Polisi lakini pia kila mmoja atakuwa na kitambulisho.

“Usajili wa awali ulikuwa wa kibubu bubu kwa mfano baaadhi ya vituo vilikuwa vinamsajili mwanachama bila kumpiga picha lakini kumbukumbu zilikuwa hazifiki ngazi ya juu lakini wa sasa utakuwa wa Kidijitali kwa kuwa ofisi ya UBOJA itakuwa na kumbukumbu hizo kwenye vitabu na kwenye mfumo wa kumbukumbu wa Kompyuta”. Alifafanua Bw. Makongoro.

Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuwadhibiti watu wanaofanya uhalifu kwa mgongo wa waendesha boda boda jambo ambalo linaweza kuwaletea taswira ambayo si nzuri machoni mwa watu.

Naye mgeni rasmi wa mkutano huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba, Jeshi la Polisi linaunga mkono moja kwa moja wazo hilo la UBOJA kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti uhalifu.

Alisema hatua hii inaonyesha nia njema walionao UBOJA kwa Jeshi la Polisi katika kushirikiana na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika jiji la Arusha lakini pia mbali ya kuonyesha taswira nzuri kwa jamii itawasaidia kwa usalama wao.

Kamanda Mkumbo alisema kwa hivi sasa ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti uhalifu ni muhimu sana na kuwataka waendelee kuliunga mkono Jeshi hilo kwa kutoa taarifa mbalimbali za uhalifu hasa unaotokea maeneo yao ya kazi.

“Kwa hivi sasa wezi wengi wanapenda kuwatumia kwa kuwakodi waendesha pikipiki; kukagua eneo la kufanya uhalifu lakini pia baada ya kufanya uhalifu wanatoroka kwa pikipiki hivyo ukimgundua mtu wa namna hiyo toa taarifa haraka kwa askari yeyote unayemuamini au kwa viongozi ili tumkamate”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo.

Aliwaasa katika utendaji wao wa kazi kutoweka mbele sana pesa bali waangalie uhai wao kwanza hasa wanapoona baadhi ya abiria wanawakodisha kwa pesa nyingi na kuwapeleka maeneo tete hasa usiku kwani wengine hawana nia nzuri.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Joseph Charles Bukombe, aliwataka wananchi wote wa mkoa huu wafuate sheria za usalama barabarani kwani kwa kufanya hivyo hakuna mtu atakayewakamata.

Mkuu huyo wa Usalama Barabarani alisisitiza suala la kuvaa kofia ngumu “Helmet” kwa dereva na abiria na kusema hatakuwa na msamaha kwa mtu yeyote atakayekaidi hilo awe mtumishi wa serikali au mwendesha pikipiki za abiria na kuongeza kwamba endapo vyombo vya usafiri vitaendeshwa salama basi vitabaki salama na watu watakuwa salama na kutaja kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani inayosema “ENDESHA SALAMA HATUTAKI AJALI TII SHERIA TUNATAKA KUISHI”.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii mkoani hapa Mrakibu Msaidizi (ASP) Edith Makweli na msaidizi wake Mkaguzi wa Polisi Shabani Shabani ulihudhuriwa na washiriki 220 toka kanda tano ambao ni viongozi wa kata na vituo vya waendesha pikipiki ambapo Jiji la Arusha linakadiriwa kuwa na jumla ya vituo vya bodoa boda 400.

No comments:

Post a Comment