Friday, April 5, 2013

ARUSHA INAKABILIWA NA ONGEZEKO KUBWA LA UHITAJI WA MAJI




ARUSHA INAKABILIWA NA ONGEZEKO KUBWA LA UHITAJI WA MAJI

NA BETY ALEX
,Arusha


Jiji la Arusha linakabiliwa na changamoto ya ongezeko kubwa la uhitaji wa maji kutoka mita za ujazo 53,030  hadi mita za ujazo 93,270 kwa siku  kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu inayokua kwa kasi isiyoendana na kiwango cha uzalishaji wa maji.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na maji taka Arusha (AUWSA) mhandishi Ruth Koya katika Kilelecha Wiki ya maji iliyoadhimishwa Jijini hapa Mwishoni mwa wiki

Alisema  kuwa Kiwango cha uzalishaji wa maji  kimeshuka kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyosababisha ukame  na kiwango hicho kushuka hadi kufikia mita za ujazo 32,000 hadi 45,000 kwa siku,hali hiyo inailazimu mamlaka husika kuwa na mgao wa maji hasa katika maeneo yaliyoinuka na yale yaliyoko pembezoni mwa jiji  kama Mbauda,Ngusero,Sombetini,Morombo na Terrat.


Mhandisi Koya aliendelea kwa kusema kuwa hali hiyo inasababishwa na ukuaji wa mji wa Arusha kutokana na kuongezeka  kwa shughuli za kijamii na za kiserikali.Hivyo kwa ujumla mamlaka yake inakabiliwa na changamoto ya kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya maji ili kukidhi ongezeko  kubwa la mahitaji ya maji.

Mbali na hayo alisema kuwa  mamlaka hiyo imekuwa na mikakati ya muda mrefu na muda mfupi ya kukabiliana na ongezeko la uhitaji wa maji kama vile uendelezaji wa chem chem za Machare zilizoko kata ya Moshono ambazo mamlaka inaendelea kuiboresha inatoa lita 30,000 kwa saa, pamoja na kuchimba visima vipya katika kata ya Sokon 1,Engutoto na Sombetini.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo,Mkurugenzi huyo amesema kuwa  wananchi wamekuwa wakivamia  maeneo ya vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli za kibinadamu  kama vile kilimo,ufugaji,uvunaji miti,uharibifu wa mazingira kwa ujumla.


Naye  Mwenyekiti wa bodi  wa mamlaka hiyo bwa  Felix Mrema alisema kuwa vyanzo vya maji vinazidi kupungua kila siku na mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka na kueleza kuwa suluhu ya tatizo hili ni serikali kufanya jitihada za makusudi  za kuyahifadhi maeneo ya vyanzo yasiingiliane na shughuli za binadamu akitolea mfano eneo la Burka na Ngaramtoni ambalo amedai kuwa  linaweza kutosheleza mahitaji ya maji kwa jiji la Arusha kwa miaka 50 ijayo.


 Aliwataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha kuwa wanajiwekea utaratibu wa kueshimu zaidi vyanzo vya maji na kuachana na tabia ya kuharibu vyanzo hivyo kwani uharibifu huo mara nyingine ndio chanzo kikubwa cha ukame ndani ya Jiji la Arusha

No comments:

Post a Comment