Tuesday, January 1, 2013

SERIKALI YASHAURIWA KUWEKEZA ZAIDI KWENYE MABADILIKO YA TABIA NCHI

Na Queen Lema,MONDULI

SERIKALI imeshauriwa kuelekeza nguvu zake na kuweka kipaumbele zaidi
katika swala  la  mabadiliko ya tabia ya nchi,ili wananchi waweze
kupata elimu ya kutosha na kuweza kukabilina na hali hiyo.


Hayo yalisemwa na  mkazi wa monduli ,Elibariki Mollel   wakati
akichangia mada  katika mdahalo wa umma juu ya athari za mabadiliko ya
tabia ya nchi, mbinu na namna ya kukabiliana na  kuendana na hali hiyo
katika jimbo la Monduli ulioandaliwa na mtandao wa asasi binafsi mkoa
wa Arusha(ANGONET).


Alisema kuwa, ili serikali iweze kukabiliana na hali hiyo ni lazima
ihakikishe kuwa inawekeza nguvu za kutosha katika swala hilo kama
inavyowekeza kwenye maswala mengine ya kijamii, ikiwa ni pamoja na
kubuni mikakati madhubuti katika kutunga sera zitakazowezesha
kukabiliana na janga hilo.


Aliongeza kuwa, wananchi walio wengi hususani waishio vijijini
wanahitaji kupatiwa elimu hiyo kwa kina kwani ndio waathirika wakubwa
wa janga hilo kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu jinsi ya
kuchukua tahadhari  wakati wa janga hilo ikiwemo kutoharibu mazingira
ambayo yanachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kiasi
kikubwa.


Naye Mratibu wa ANGONET mkoa wa Arusha, bw Peter Bayo alisema kuwa,lengo
la mdahalo huo ni ili kuwashirikisha wananchi mbalimbali waweze kutoa
maoni yao juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kupatiwa elimu
juu ya hali hiyo ili waweze kuishi kulingana na hali ilivyo hivi sasa.


Alisema kuwa,baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi na mabadiliko ya
tabia ya nchi ni sekta ya kilimo , mifugo na usalama wa chakula huku
ikilinganishwa kuwa kilimo ni sekta muhimu katika kuwezesha ukuaji wa
uchumi na ustawi wa jamii.


Alisema kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wamejiajiri katika
kilimo ,na ni wazi kuwa sehemu kubwa imeathiriwa sana na ukame
kutokana na kubadilika kwa majira ya mvua.

Bayo aliongeza kuwa, mabadiliko ya tabia ya nchi yamechangia kwa kiasi
kikubwa sana kupotea kwa makazi ya viumbe hai ,ambapo asilimia 20-30
ya viumbe hai wanaounda sehemu ya bioanuai  wako hatarini kutoweka
kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

MWISHO

No comments:

Post a Comment