Tuesday, April 29, 2014

MANYARA WAPEWA CHANGAMOTO YA MABWENI

ILI kupambana na changamoto za elimu kwa watoto wa kike Mkoani Manyara, imeelezwa suluhisho ni kuwajengea mabweni ya kulala kwani hivi sasa wanasoma kwenye mazingira mabovu kutoka na mazingira ya mkoa huo.
 
Wito huo umetolewa Wilayani Mbulu na Mwenyekiti wa Mtandao wa asasi za kiraia mkoani Manyara, (Macsnet) Asia Lembariti, wakati akizungumza juzi kwenye Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
 
Lembariti alisema ili kuboresha elimu kwa mtoto wa kike shirika la WEGCC limejikita kufanya utafiti kwenye sekta ya elimu hasa ubora wa mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike katika shule za sekondari.
 
Alisema shule nyingi zipo mbali na kaya nyingi wanakotoka wanafunzi na uhaba wa miundombinu unachangia wanafunzi kutembea umbali mrefu mpaka kilometa 16 hadi 32 kwa siku, kwenda shule na kurudi nyumbani.
 
“Hii ni hatari zaidi kwa watoto wa kike na suluhisho ni mabweni, kwani huchangia mahudhurio hafifu, kuacha shule, kuchochea ubakaji na ujauzito kwani toka mwaka 2004 hadi 2010 watoto 45,256 waliacha masomo,” alisema.
 
Alisema ili kukabiliana na changamoto zote hizo zisababishwazo na kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shule, ujenzi wa mabweni ni muhimu, tofauti na kupanga kwenye magheto na matatizo kwenye vyombo vya usafiri kila siku.
 
Alisema Macsnet inatekeleza miradi minne kwa kushirikiana na wanachama wake ndani ya mkoa huo ikiwemo kuboresha elimu kwa watoto wa kike kuwajengea uwezo wa uandishi wa miradi, kuboresha ufugaji wa asili na kuboresha lishe.
 
“Katika kufanikisha miradi hiyo Wegcc imejikita kufadhili mradi wa kuboresha elimu kwa watoto wa kike na pia tunashirikiana na Usaid katika lishe, Care International kwa ufugaji na FCS utekelezaji miradi,” alisema Lembariti.
 
MWISHO.

No comments:

Post a Comment