Tuesday, May 27, 2014

Wanafunzi 125 kushiriki Riadha manyara



Wanafunzi 125 wa michezo ya riadha, mpira wa miguu, pete na wavu, wa shule za sekondari Wilaya ya Hanang’ wanatarajia kushiriki mashindano ya umoja wa michezo ya shule za sekondari (Umiseta) Mkoani Manyara.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, mratibu wa umiseta wilayani humo, Caroline Marshali alisema wavulana na wasichana wa shule tofauti za sekondari wanashiriki michezo mbalimbali ya kutafuta wawakilishi wa wilaya hiyo.

Marshali alisema wanafunzi hao wa shule za sekondari watawakilisha wilaya hiyo kwenye kuruka juu, chini, kutupa mkuki, sahani, tufe, mbio ndefu na za mita 100, 200, 400, 800, 1,500 na mbio ndefu za marathoni.

“Pia kutakuwa na timu za mpira wa miguu za wasichana na wavulana, mpira wa wavu na mpira wa pete na wachezaji wetu wamejiandaa ipasavyo kwenye mashindano haya ili kuipa sifa wilaya yetu,” alisema.

Naye, Mwenyekiti wa umoja wa wakuu wa shule za sekondari (Tahosa) wilayani Hanang’ John Malley alisema wamewaandaa ipasavyo vijana wao ili washiriki kikamilifu michezo hiyo na kuleta ushindi katika wilaya yao.

“Pamoja na hayo tunamshukuru Mbunge wa jimbo letu Mary Nagu kwa kutuunga mkono kwenye maandalizi haya ya kwenda kushiriki mashindano ya mkoa kwa ikiwemo kutupa vyakula,” alisema Malley.

Nao baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu, wavu na kuruka juu, Nobert Aushak, Judith Mkilanya na Anna Aney walisema kupitia michezo wanajijenga kisaikolojia ili wafanikiwe katika masomo yao kwani hawana hofu ya mitihani.

Walidai kuwa zaidi kufahamiana na watu mbalimbali kupitia michezo, pia wanajenga afya zao kwa kuwa wakakamavu na wanajiamini zaidi pindi wakiwa masomoni hivyo wanatarajia kufanikiwa pia kimasomo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment