Tuesday, May 27, 2014

HOSPITALI YA MT MERU ARUSHA YAENDELEA KUKABILIWA NA CHANGAMOTO

HOSPITALI ya Mkoa  wa Arusha, Mount Meru, inakabiliwa na upungufu wa
shuka 300 na blanketi 200, kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa kila
siku.

Akizungumzia upungufu huo jana hospitalini hapo, wakati akipokea
msaada wa shuka nyeupe 100 na blanketi 30 toka kwa Kanisa la Calvary
Temple la Kilombero Jijini Arusha,ambalo linaadhimisha miaka 75 tangu
lianzishwe, Mganga Mfawidi wa Hospitali hiyo, Dk. Josiah Mlay, alisema
upungufu ni mkubwa wa vitu hivyo ukizingatia wanakwenda kipindi cha
baridi kali.

Alisema kuwa shuka na blanketi walizonazo kwa sasa nyingi zimechakaa
kutokana na kemikali wanazotumia kufulia wakati zinapochafuka wodini,
hivyo wanahitaji shuka na blanketi zingine haraka kabla ya msimu wa
baridi haujaanza.

"Kwa nyie kutuletea hivi vitu tunashukuru sana na mtabarikiwa, kwani
bado tuna upungufu wa itu hivi mkubwa na tunaomba wadau wengine
wajitokeze kutusaidia kabla ya msimu wa baridi haujaanza,"alisema.

Dk. Mlay alisema kwa sasa hospitali hiyo inachangamoto kubwa ya
ongezeko la wagonjwa na huku mahitaji yao yakipungua, kutokana na
wingi wao, hivyo wanahitaji wasamaria wema wajitokeze kuwasaidia.
Mahitaji mengine wanayohitaji hospitalini hapo alitaja kuwa pamoja na
vifaa vya maabara navyo ni vichache,hivyo wanaomba msaada kwa
wasamaria wema na sio kuiachia serikali ambayo inamajukumu mengi.
Kwa upande wake Emmanuel Mbwiga ambaye ni Mzee wa  Kanisa la Calvary

Temple la Kilombero Jijini Arusha, akitoa msaada huo alisema mbali na
msaada huo pia kupitia vituo vyao mbalimbali wametoa msaada kwenye
vituo vya yatima vya Huruma Kwamurombo,Monduli,Esso.

Pia misaada mingine imetolewa shule za msingi Mwangaza, Olsinyai
Sombetini na Ngarenaro, lengo kubwa kusaidia watu wenye shida ili
wapate faraja nao katika kuadhimisha kilele cha kanisa hilo
kitakachofanyika Kitaifa Mbeya Julai mwaka huu.

Mbwiga alisema vitu walivyotoa maeneo hayo  ni Sabuni, ndoo za mafuta,
mchele, nguo, mahindi,daftari,soksi na vitu vingine vingi, ambavyo
vyote vina jumla ya shilingi milioni 3.

 Hata hivyo alitoa wito kwa watu wenye mapenzi mema kujitokeza
kusaidia hospitali hiyo na maeneo yenye uhitaji kama vitruo vya yatima
na shuleni, ili wabarikiwe zaidi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment