Sunday, September 29, 2013

GAZETI LA MTANZANIA LAFUNGIWA KWA SIKU 90 MWANANCHI SIKU 14

SERIKALI kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) imelifungia Gazeti la MTANZANIA kwa muda wa siku 90 kupitia Tangazo la Serikali namba 332 la tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kile inachodai kuwa limekuwa likiandika habari za kichochezi. Sambamba na MTANZANIA, pia imelifungia gazeti la MWANACHI kwa muda wa siku 14 kwa madai hayo hayo.

Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Assah Mwambene, kwa vyombo vya habari vichache vilivyotumiwa wito wa kuwepo kwa mkutano baina yake na vyombo hivyo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mwambene, ilisambazwa pia katika mitandao ya kijamii na ilieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kulionya mara nyingi MTANZANIA kuacha kuandika habari za uchochezi lakini halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti.

Ilizitaja habari inazodai kuwa za uchochezi kuwa ni pamoja na iliyochapishwa katika toleo namba 7262 la Machi 20 mwaka huu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘URAIS WA DAMU,’ na makala ya uchambuzi iliyochapishwa Juni 12 katika toleo namba 7344 iliyokuwa na kichwa cha maneno ‘MAPINDUZI HAYAEPUKIKI.’

Habari nyingine iliyolalamikiwa na serikali ni iliyochapishwa Jumatano ya Septemba 18 mwaka 2013 katika ukurasa wa mbele wa toleo namba 73414 iliyobebwa na kichwa kisemacho ‘SERIKALI YANUKA DAMU.’

Taarifa ya Mwambene inadai kuwa habari hiyo ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta na kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.

Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa habari hiyo haikuwa na uthibitisho na ililituhumu Jeshi la Polisi kuhusika na wahanga walioumizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya na pia kuishitumu serikali kwa ugoigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.

Kwa upande wa Gazeti la MWANANCHI, serikali imeeleza kuwa imechukua uamuzi wa kulifungia kwa sababu ya kuandika habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani na imetoa mfano wa habari iliyokuwa na kichwa kisemacho MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013 na nyingine iliyokuwa na kichwa kilichosomeka ‘WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI.’

No comments:

Post a Comment