Monday, May 6, 2013

Kamati ya maendeleo ya Mirerani yatembelea nyumba 26 zilizoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha


Diwani wa kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,Justin Nyari akikagua nyumba ya mkazi wa mtaa wa Songambele,Katarina Selemani iliyoanguka kutokana na mafuriko yaliyotokea juzi na kuathiri baadhi ya nyumba na mazao ya wakazi wa kata hiyo.picha na Queen Lema,Simanjiro








                                     




Kamati ya maendeleo ya Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa sehemu tofauti hapa nchini.

Akiongoza msafara huo juzi,Diwani wa kata ya Mirerani Justin Nyari aliwapa pole waathirika wa mafuriko hayo ambapo nyumba zaidi ya 26 na mazao mbalimbali yaliathirika kutokana na mafuriko hayo.

Akizungumza na baadhi ya waathirika hao,Nyari alisema ameshatoa taarifa kwa Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro,Patrice Saduka kwa ajili ya hatua zaidi ya kutatua tatizo hilo.

“Hatua ya kwanza tuliyochukua na WDC yangu ni kutembelea na kubaini sehemu zilizoathirika na kutoa taarifa wilayani na watamtuma mhandisi Agai,lakini kubwa zaidi mji wa Mirerani unapaswa upimwe,” alisema Nyari.

Hata hivyo,Diwani wa kata hiyo Nyari alimkabidhi kifuta machozi cha fedha mmoja kati ya waathirika wa mafuriko hayo,Katarina Selemani mkazi wa Songambele ambaye nyumba aliyokuwa anashi ilibomolewa na mafuriko hayo.

Naye,mwathirika mwingine wa mafuriko hayo Boniface Mboya,akizungumza mbele ya kamati hiyo alisema mafuriko hayo yameathiri eneo analoishi kwani miti 750 ilichukuliwa na mafuriko,miche 1,300 na maua 250 na choo kubomoka.

Baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo walidai kuwa,mvua kubwa zilizonyesha kwenye maeneo tofauti ya mkoa wa Arusha,yamesababisha mafuriko hayo yaliyopitia Msitu wa Mbogo,Mbuguni hadi eneo hilo na kuelekea Majengo.

MWISHO.





No comments:

Post a Comment