Thursday, January 30, 2014

SERIKALI YAJITOSA ARUSHA KWA KULIPA FIDIA


Na Queen Lema, Arusha

SERIKALI imefanikiwa kutoa kiasi cha Bilioni moja na Milioni 750 kama fidia kwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha mara baada ya kuchukua mradi wa Halmashauri hiyo ujulikao kama Laki Laki kwa ajili ya kujenga miji ya kisasa zaidi.

Akidhibitisha mbele ya kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri mkurugenzi mtendaji Bw Fidelis Lumato alisema kuwa mpaka sasa wameshapokea fidia hiyo ya mradi wa mashamba ya Laki laki ambao ulikuwa chini ya Halmashauri hiyo .

Lumato alisema kuwa pamoja na kuwa mpaka sasa wameshaweza kuachia mradi huo na kutoa kwa Serikali kuu lakini fidia hiyo itasaidia sana kuweza kufanya marekebisho ndani ya Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kununua mahitaji ya msingi.

Alidai kuwa fidia hiyo imeweza kurahisisha kazi mbalimbali za halmashauri kwa kuwa yapo mahitaji ya msingi ambayo yalikuwa yanahitajika lakini hapakuwa na jinsi ya kupata fedha kwa ajili ya kununua jambo ambalo wakati mwingine lilikuwa linasababisha malengo kukwama.

Aidha alitaja vitu ambavyo vitaweza kununuliwa kutokana na fidia hiyo kuwa ni pamoja na Gari kwa ajili ya matumizi ya shule za sekondari katika Halmashauri hiyo,tipper  kwa ajili ya shuguli za ujenzi ambapo pia nalo litachangia mapato ya halmashauri hiyo.

Vitu vingine ambavyo vitafanyika kutokana na fidia hiyo ni pamoja na ukarabati wa jengo la kisasa la Halmashuri hiyo ambalo bado halijaweza kukamilika rasmi kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri hiyo.

“tunashukuru mungu serikali kutupa fidia ya mradi wa mashamba ya Lakilaki kwani kwa kipindi cha mwaka huu tutafanya vitu vingi na tunaimani kabisa hata mapato nayo yataweza kuongezeka zaidi na hivyo kuwasaidia hata wananchi wenyewe”aliongeza Lumato.

Awali Kaimu Mweka hazina wa Halmashauri hiyo ambaye ni bw Munguabella Kakulima alidai kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuweza kuongeza vyanzo vya mapato kwani mpaka sasa kuna tofauti kubwa sana ya ongezeko la mapato katika Halmashauri hiyo ya Arusha Vijijini .

Kakulima alidai kuwa hapo awali waliaanza na mapato ya Milioni 400 lakini mpaka sasa wameweza kufikia ukusanyaji wa mapato wa zaidi ya Bilioni 2 jambo ambalo lengo lake ni kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inaepukana na tabia ya kuwa tegemezi.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment