Thursday, January 30, 2014

MANYARA WAPEWA JEZI

Na GLADNESS MUSHI, Manyara

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara, Mohamed Omary Farah, amegawa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh600,000 kwa timu mbili za soka za Mrara FC na Waangwaray FC za kata ya Babati.
 
Akigawa vifaa hivyo jana kwenye uwanja wa Mrara uliopo mjini Babati, Farah ambaye pia ni Diwani wa kata ya Babati alisema lengo la kugawa vifaa hivyo ni kuhakikisha sekta ya michezo inapiga hatua katika eneo hilo.
 
Alisema anatoa msaada huo wa vifaa vya michezo kwa lengo la kuwaendeleza ambapo timu hizo mbili zilipatiwa kila moja seti moja ya sare za michezo ikiwemo tisheti, bukta na soksi pamoja na mpira mmoja.
 
Alisema kupitia michezo vijana wataweza kujinufaisha kwani hivi sasa michezo ni ajira na pia wataweza kujiweka pembeni na mambo mabaya ikiwemo tabia za uhuni na uvutaji dawa za kulevya.
 
Alisema atahakikisha anakuwa nao sambamba katika michezo kwenye kuwaunga mkono ili timu hizo ziweze kufika madaraja ya juu na kuzileta timu kubwa kwenye mji huo wa Babati.
 
Hata hivyo, mwakilishi wa timu ya Mrara FC Gerald Romly akitoa shukrani kwa niaba ya timu hizo alisema watatumia msaada huo wa vifaa vya michezo kwa kuzitumia ipasavyo kwa ajili ya lengo la kufanikisha michezo.
 
Romly alimshukuru Farah kwa kuwapa msaada huo wa michezo na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano wake, kwani ameonyesha moyo na kujali michezo inayofanywa na vijana wa eneo hilo.
 
MWISHO.

No comments:

Post a Comment