Saturday, October 26, 2013

Wafanyakazi wa hoteli hawana ujuzi na elimu ya kutosha.


,Arusha.
IMEELEZWA kuwa asilimia kubwa ya watanzania wamekuwa  hawapati nafasi mbalimbali za ajira kwenye mahoteli kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu  ya kutosha na hivyo kuchangia wageni kutoka nje ya nchi kupata ajira kwa urahisi .

Aidha hali hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa sana vijana wengi kukosa ajira katika mahoteli kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya  vitendo na hivyo kuishia kutumia elimu ya darasani.

Hayo yalisemwa jana na  Meneja wa programu  wa shirikisho la vyama vya utalii Tanzania (TCT)  Fatma Mabrouk  alipokuwa akizungumza na wamiliki wa mahoteli jijini Arusha wakati wa kuutambulisha programu ya mafunzo  kazini ambayo itawanufaisha vijana wenye umri wa miaka 17-25.

Alisema kuwa, programu hiyo kwa sasa ipo katika hatua ya majaribio  kwa miaka miwili ambapo wameanzia jijini Dar es Saalamu kwa kuzungumza na wamiliki  wa  mahoteli kwa lengo la kuitambulisha programu hiyo ili waweze kuitumia kwa wafanyakazi  wao na kuongeza ufanisi na utendaji kazi zaidi.

Fatma aliongeza kuwa,programu hiyo itasaidia kuwaongezea wafanyakazi wa mahoteli ujuzi zaidi katika utendaji kazi wao kwani wengi wao hawana ujuzi  huo hali inayochangia wengi wao kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

‘kwa sasa hivi wengi wao wanajifunza masomo ya darasani kwa asilimia 70 huku makazini wakitumia asilimia 30 tu, hali ambayo inaadhiri utendaji kazi wao kwa kiasi kikubwa kutokana na kutumia muda mwingi darasani badala  ya makazini’alisema Fatma.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa chama cha mahoteli  Tanzania(HAT) ,alisema kuwa,Lathifa Sykes alisema kuwa,baada ya muda majaribio kumalizika programu hiyo itapitishwa kuwa sheria na hatimaye kuweza kutumika katika vyuo mbalimbali vya utalii hapa nchini .

Sykes aliongeza kuwa,kwa sasa vyuo vingi vya utalii vimekuwa vikitoa elimu hiyo kwa njia tofauti tofauti na hivyo kupitia programu hii itasaidia kufundisha kitu kimoja kwa vyuo vyote na hivyo kuwawezesha wanafunzi hao kupata ujuzi unaohitajika katika soko la hoteli.

Alisema kuwa,programu hiyo inafadhiliwa na shirika la kazi duniani (ILO) ambapo lengo halisi ni kuhakikisha kuwa idadi ya wafanyakazi kwenye mahoteli inaongezeka .
Mwisho.

No comments:

Post a Comment