Monday, January 2, 2012

MORANI WA KIMASAI WAVUNJA NA KUHARIBU KANISA, FAMILIA TANO ZAKIMBIA MAKAZI YAO KWA KOSA LA KUFANYA TOHARA KISASA, NA KUSALI



Katika hali isiyokuwa ya kawaida Vijana wa kundi la Kimasai wajulikano kama ‘Morani” wameamia kanisa la T.AG. oljoro Jerusalem na kuvunja kanisa hilo kwa madai kuwa sala pamoja na vitendo pamoja na Imani ambazo wanazo baadhi ya waumini wa kanisa hilo zina haribu Mila na Desturi ya kabila hilo la wamasai.

Hali hiyo ilitokea wiki iliyopita ambapo morani hao walivamia kanisa hilo na kuharibu sanjari na kuwatafuta baadhi ya waumini wa kanisa kwa malengo ya kuwatembeza mitaani uchi pamoja na kuwatoza faini ya pesa na faini ya Ngombe dume kwa kosa la kuharibu Mila na Desturi ya Kimasai.

Akiongea kijijini hapa msimamizi wa Makanisa ya T.A.G katika maeneo hayo Mchungaji Simion Vomo alisema kuwa kutokana na imani za morani hao, kanisa limelazimika kuchukua hatua kali na za kisheria juu ya Vurugu ambazo zinafanywa  na watu hao

Mchungaji Vomo alieleza kuwa Morani hao wamekuwa wakifanya hivyo kwa kuhofia kuwa baadhi ya waumini ambao wanajua madhara ya kuabudu na kukumbatia mila anbazo zinamchafua Mungu hivyo wanaamua kuwafuata watumishi  na kisha kuwatembeza uchi mitaani

Alisema kuwa mpaka sasa familia kama tano zimelazimika kukimbia kijijini hapo kwa kuhofia usalama wa maisha yao na familia zao kwa kuwa Morani hao wameshatangaza vita dhidi yao ya kuwatembeza mitaani wakiwa uchi kama fundisho kwa baadhi ya watu ambao watakaondelea na sala sanjari na kufanya tohara kwa njia za kisasa zaidi.

“tunayoongea sasa ndugu mwandishi ni kwamba mpaka sasa familia kama tano zimekimbia makazi yao ya kudumu kwa kuwa wanahofu ya hawa morani na kisa kikubwa ni imani zao katika kuomba , kukataa hii mila ya kufanya tohara kwa njia za kienyeji sana, na kukataa kuabudu Mila za kimasai”alieleza mchungaji Vomo.


Pia alisema kuwa mara baada ya kanisa kuona hali kama hiyo walilazimika kutumia njia na busara za kisasa zaidi za kuweza kuwaelimisha Morani hao, lakini morani hao walionekana kukiuka makubaliano hayo na ndipo walipovamia kanisa hilo pamoja na kumkamata muumini mmoja ambaye alirejea kijjini hapo mara baada ya kuwepo kwa muafaka

Alibainisha kuwa Morani hao walifanikiwa kuvunja mlango kwa muumini huyo ambaye yeye anatuhumiwa kwa kosa la kufanya ibada na kukiuka mila hizo za kimasai  majira ya usiku wa saa sita ambapo ilikuwa ni December 30 na kumtembeza umbali mrefu ambapo alitembea kwa masaa kama sita  jambo ambalo si sahihi hata mbele za Mungu.

“fikiria hali ya usiku ilivyokuwa alafu unamtembeza mtu akiwa amevaa gunia kisa ni imani yake ambayo inatoka katika biblia kisha unadai fedha na Ngombe kweli hii ni halali tutahakikisha kuwa tunapambana na hili mpaka tukomeshe hili tatizo’alisema mchungaji Vomo.

Katika hatua nyingine msimamizi wa makanisa hayo alisema kuwa ni lazima sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha hali kama hiyo ambayo kwa sasa imeonekana kukua sana ndani ya mkoa wa Arusha kwa kuwa baadhi ya Masai wanataka Tohara kwa njia ya Kienyeji sanjari na kupinga makanisa yenye kukataa imani hiyo.

Awali Familia ambazo zimekimbia kutokana na kutafutwa na Morani hao zilisema kuwa kamwe hawataweza kukubaliana na wanachokitaka na kudai Morani hao kwa kuwa Biblia haijaonesha sehemu za kuabudu mila na desuri kama zao.

“hata kitokee nini sisi hatubadilishi msimamo wetu na badala yake tutazidi kumtangaza yesu kuwa mshindi wetu na pia kila kinachofanyika kimbilio letu ni Biblia na wala sio maagano, Mila, na Desturi”zilisema Familia hizo.

Nao Morani ambao walizunguka Kanisa hilo December 31 walisema kuwa ili mambo yaende vema wakati wkisubiri upatanishi baina ya familia hizo tano na kanisa, wanataka Kanisa hilo la T.A.G Oljoro Jerusalem Lifungwe hali ambayo Msimamizi wa Makanisa hayo alikataa na kusema kuwa ibada na taratibu zake itaendelea kawaida na kamwe hawatasitisha  kwa kosa la Mila.

Nae Kaimu Kamanda wa polisi kwa mkoa wa Arusha Bw Akili Mpwapwa alisema kuwa bado wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ambapo watakaohusika kufanya fujo, kuchukua mali za watu au kuharibu kama walivyo fanya watafikishwa mahakamani kwani hayo ni makosa ya jinai.

MWISHO 

CHANZO CHA HABARI NA QUEEN LEMA

ARUSHA 

0758907891.

No comments:

Post a Comment