Joseph Ngilisho,Arusha
BARAZA la michezo Tanzania BMT,limewataka wadau wa
michezo kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki program inayolenga kukusanya
maoni juu ya rasimu ya namna ya kuhamasisha na kuendeleza michezo shirikishi hapa nchini .
Akizungumza kwenye warsha ya kukusanya maoni jijini
Arusha,Afisa mwandamizi wa BMT ,John Chalukulu alisema kuwa lengo la kukusanya
maoni kwa wadau wa michezo hapa nchini ni kuhakikisha kuwa michezo inapendwa na
jamii kwani kwa kiwango kikubwa jamii imeipa kisogo.
Alisema kuwa kwa sasa kumekuwepo na mwamko hafifu kwa
jamii kuhusu suala la michezo na kwa kubaini hilo wameamua kuanzisha midahalo
katika mikoa mitano hapa nchini itakayowakutanisha wadau wa michezo ili kubaini
jamii inahitaji nini kukuza michezo hapa nchini.
Akizungumzia hali ya kudorora kwa sekta ya michezo hapa
nchi alisema kumekuwapo na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa fedha,mwamko
hafifu wa kushiriki michezo,wananchi kupenda michezo ya aina moja nk,ukosefu wa
viwanja vya michezo pamoja na vifaa.
Kwa upande wa mgeni rasmi katika warsha hiyo,Sifael Ole
Ngashwa Mollel ambaye ni kaimu katibu tawala wa wilaya,alilitaka baraza hilo la
michezo nchini kujikita kuhamasisha zaidi michezo mashuleni ili jamii ione
umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye sekta hiyo.
Alisema kuwa, swala la michezo linapaswa kufanyika kwa
umakini zaidi huku wakiwafikia walengwa ambao ni wanafunzi wa shule za msingi
,vyuo vikuu na taasisi zote ili kuwezesha kupata wataalamu katika ngazi zote na
hatimaye kuwezesha elimu ya michezo kuenea ngazi zote.
‘’pelekeni walimu
wa michezo mashuleni na muongeze hamasa ili jamii ianze kuona umuhimu wa kutoa
kipaumbele masuala ya michezo kwa vijana na makundi mengine kwani hivi sasa
michezo imezorota sana mashuleni kutokana na kutokuwa na walimu wenye uzoefu wa
kutosha ambao wana uwezo wa kutoa elimu hiyo’’alisema.
Aliongeza kuwa, swala la michezo katika shule mbalimbali
hivi sasa limekuwa likifanyika kwa kuigiza hali
ambayo imechangia kupotea kwa maana halisi ya michezo mashuleni ,hivyo
baraza hilo lina changamoto kubwa kuhakikisha kuwa linajiwekea mikakati na
utaratibu mzuri wa kuandaa michezo mashuleni .
Mollel aliongeza kuwa, umefika wakati sasa wa
halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinashirikiana na baraza hilo kutatua
changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa viwanja, katika shule mbalimbali
za msingi ili kuwezesha wanafunzi kupata haki zao za msingi.
BMT,tayari imeshaifikia mikoa ya Zanzibar,Mwanza na Arusha ikifuatiwa na mikoa ya Songea na Dar es salaam.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment