ARUSHA INAKABILIWA NA ONGEZEKO KUBWA
LA UHITAJI WA MAJI
NA BETY ALEX,Arusha
Jiji la Arusha linakabiliwa na
changamoto ya ongezeko kubwa la uhitaji wa maji kutoka mita za ujazo
53,030 hadi mita za ujazo 93,270 kwa siku kutokana na ongezeko
kubwa la idadi ya watu inayokua kwa kasi isiyoendana na kiwango cha uzalishaji
wa maji.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi
na maji taka Arusha (AUWSA) mhandishi Ruth Koya katika Kilelecha Wiki ya maji
iliyoadhimishwa Jijini hapa Mwishoni mwa wiki
Alisema kuwa Kiwango cha uzalishaji wa maji
kimeshuka kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyosababisha ukame
na kiwango hicho kushuka hadi kufikia mita za ujazo 32,000 hadi 45,000 kwa
siku,hali hiyo inailazimu mamlaka husika kuwa na mgao wa maji hasa katika maeneo
yaliyoinuka na yale yaliyoko pembezoni mwa jiji kama
Mbauda,Ngusero,Sombetini,Morombo na Terrat.
Mhandisi Koya aliendelea kwa kusema
kuwa hali hiyo inasababishwa na ukuaji wa mji wa Arusha kutokana na
kuongezeka kwa shughuli za kijamii na za kiserikali.Hivyo kwa ujumla
mamlaka yake inakabiliwa na changamoto ya kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya
maji ili kukidhi ongezeko kubwa la mahitaji ya maji.
Mbali na hayo alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa na mikakati ya muda
mrefu na muda mfupi ya kukabiliana na ongezeko la uhitaji wa maji kama vile
uendelezaji wa chem chem za Machare zilizoko kata ya Moshono ambazo mamlaka
inaendelea kuiboresha inatoa lita 30,000 kwa saa, pamoja na kuchimba visima
vipya katika kata ya Sokon 1,Engutoto na Sombetini.
Akizungumzia changamoto
zinazoikabili mamlaka hiyo,Mkurugenzi huyo amesema kuwa wananchi wamekuwa
wakivamia maeneo ya vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli za
kibinadamu kama vile kilimo,ufugaji,uvunaji miti,uharibifu wa mazingira
kwa ujumla.
Naye
Mwenyekiti wa bodi wa mamlaka
hiyo bwa Felix Mrema alisema kuwa vyanzo
vya maji vinazidi kupungua kila siku na mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka na
kueleza kuwa suluhu ya tatizo hili ni serikali kufanya jitihada za
makusudi za kuyahifadhi maeneo ya vyanzo yasiingiliane na shughuli za
binadamu akitolea mfano eneo la Burka na Ngaramtoni ambalo amedai kuwa
linaweza kutosheleza mahitaji ya maji kwa jiji la Arusha kwa miaka 50 ijayo.
Aliwataka wananchi wa Mkoa wa
Arusha kuhakikisha kuwa wanajiwekea utaratibu wa kueshimu zaidi vyanzo vya maji
na kuachana na tabia ya kuharibu vyanzo hivyo kwani uharibifu huo mara nyingine
ndio chanzo kikubwa cha ukame ndani ya Jiji la Arusha
No comments:
Post a Comment