Wednesday, December 4, 2013

ACHENI UKIRITIMBA USIOKUWA WA LAZIMA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, amewataka watumishi wa
serikali na taasisi zake kuondoa ukiritimba usio wa lazima katika
kutoa huduma kwa wadau wa maendeleo, hususani, wanaowafundisha
wakulima wadogo wadogo  kilimo cha kibiashara ili waweze kujipatia
maendeleo.




Alitoa maagizo hayo wakati akifungua maonesho ya vikundi vya wakulima
zaidi ya 21 kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, yaliyoandaliwa na
Shirika lisilo la kiserikali la Farm Concern International (FCI)
wakishirikiana na World Vision Tanzania, World Vision Canada na
Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA), jijini hapa jana.




Mkurugenzi wa FCI Afrika, David Richiu, alisema shirika lake ambalo ni
wakala wa masoko kwa wakulima wadogo wadogo, limejikita kuwafundisha
kilimo cha kibiashara, uongozi katika vikundi kupitia mfumo kijiji
biashara, wanawapa mbinu za kutafuta masoko ya mazao, utunzaji wa
mazingira, elimu ya lishe bora kwa familia, uhifadhi wa mazao,
huwaunganisha na watu wa pembejeo na huduma za ugani.



Alisema maonesho hayo ya kilimo yenye kauli mbiu, “Jua mahitaji ya
soko zalisha kibiashara,” yamedhaminiwa na mradi wa SMART (Sustainable
Market led Agriculture Resource) na wanafanya kazi katika wilaya za
Arusha, Monduli, Siha, Arumeru na Hai.



Baadhi ya miradi ambayo shirika lake linatekeleza nchini ni pamoja na
kukuza uzalishaji na ulaji wa mboga mboga za kiasili unaotekelezwa
katika wilaya za Arusha, Arumeru, Hai, Siha, Same na Karatu, lishe kwa
wakulima wa kahawa unaotekelezwa wilaya za Arusha, Arumeru, Siha na
Hai.



Mingine ni mradi wa muhogo ulioanzia kijiji cha Mbuguni wilayani
Arumeru, mradi wa ndizi na viazi vitamu hasa viazi lishe vyenye
asilimia nyingi ya vitamin A ambao wanatarajia kuupanua kwenye mikoa
mingine nchini.



Kwa upande wake, Kiongozi mkazi wa FCI nchini, Wiston Mwombeki,
alisema ili mkulima aweze kupata soko yampasa kwanza ajue mahitaji ya
soko kama vile mazao yanayohitajika sokoni, ubora, mahali walipo
wanunuzi, kiwango kinachotakiwa, ufungashaji, uhifadhi na usafirishaji
wa mazao, kilimo bora na pembejeo bora.


MWISHO.

No comments:

Post a Comment