UKOSEFU WA NYUMBA ZA POLISI MERERANI CHANZO CHA UTENDAJI
HAFIFU WA POLISI
IMEELEZWA kuwa ukosefu wa nyumba za askari polisi wa
kituo cha Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara unachangia kuchelewesha
utendaji kazi wao kwani inawabidi watoke majumbani kwao na kwenda kituoni ndipo
wafike kwenye eneo la tukio.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo
wa Mirerani,Albert Siloli kwenye kikao cha siku ya familia ya polisi na wadau
wa mji huo cha kujadili tathmini ya utendaji kazi wake kwa mwaka uliopita.
Siloli alisema ukosefu wa nyumba za askari polisi
unachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha utendaji kazi wao kwani
unawachelewesha kufika kwenye tukio husika na kuchukua hatua stahili ikiwemo
kuthibiti uhalifu.
Alisema Serikali inapaswa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kwa kuwajengea
nyumba karibu na kituo cha polisi askari hao ili waweze kutimiza wajibu wao kwa
jamii ipasavyo kwani hivi sasa mji huo unazidi kupanuka kwa haraka.
Hata hivyo,kwa niaba ya wenyeviti wengine wa mitaa ya
mji mdogo wa Mirerani,Siloli alitoa pongezi kwa askari hao kwani uhalifu hivi
sasa umepungua kwa kiasi kikubwa kwenye mji wa Mireraani hivyo jamii inaishi
kwa amani ya kutosha.
Pia,Mwenyekiti huyo alimpongeza Mkuu wa kituo cha
polisi Mirerani,Mrakibu Msaidizi wa polisi Ally Mohamed Mkalipa kwa kuandaa
hafla kwani haijawahi kufanyika tangu kituo hicho kianzishwe mwaka 1998 na
utendaji kazi wao ni wa asilimia 100.
Pamoja na hayo alisema baadhi ya askari wa usalama
barabarani wanakabiliwa na changamoto ya kudaiwa kupokea rushwa kwenye kazi zao
hivyo kulitia doa jeshi hilo kwani jamii
inalalamika mno kuhusiana na jambo hilo.
Kwa upande wake,Mkuu wa kituo cha Polisi Mirerani
Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Ally Mohamed Mkalipa aliwashukuru wenyeviti wa
mitaa hao kwa kutambua kuwa uhalifu hivi sasa umepungua kwenye mji huo.
Mkalipa ameeleza kuwa jamii inatakiwa kuongeza
ushirikiano kwao kwani ni dhahiri shahiri uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa
na watajitahidi kuondokana na changamoto zinazowakabili
Kuhusu suala la baadhi ya askari polisi kuhusishwa na
upokeaji rushwa amesema watalifuatilia jambo hilo kwani maadili yanawataka askari
wasijihusishe na vitendo.
Alisema kisingizio cha kudai kuwa mshahara mdogo
unachangia polisi kupokea rushwa siyo sahihi kwani upo utafiti umebaini kuwa
hata wanaopokea mshahara mkubwa wana kawaida ya kupokea rushwa hivyo
watawachunguza na wakiwabaini watawachukulia hatua ikiwemo kuwashitaki
kijeshi,kuwafukuza kazi na kwenye mahakama za kawaida.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment