Saturday, March 9, 2013

IELIMISHENI JAMIII KUHUSU UMUHIMU WA MPANGO WA MKUHUMI- MUNASA NYIREMBE


IELIMISHENI JAMIII KUHUSU UMUHIMU WA MPANGO WA MKUHUMI- MUNASA NYIREMBE

Na Queen Lema,Arusha


VIONGOZI wa idara mbalimbali zinazohusika na Misitu hapa Nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia na wanaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mpango mkakati wa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa itokanayo na ufyekaji  na uharibifu wa misitu(MKUHUMI) ambapo mpango huo unalengo lakuokoa tani nyingi zaidi za  misitu

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,Munasa Nyirembe wakati akifungua warsha ya wadau wa mpango huo jijini hapa mapema juzi

Munasa alisema kuwa mpango huo ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi ya Tanzania pamoja na mkoa wa Arusha ingawaje kwa sasa Changamoto ni kubwa sana  hasa maeneo ya vijijini ambapo asilimia kubwa ya jamii wanafyeka misitu kwa ajili ya matumizi mbalimbali

Alisema kuwa endapo kama Kiongozi wa idara atasimama vema katika nafasi yake na kuhamisisha umma juu ya umuhimu wa mradi huu basi atachangia kwa kiwango kikubwa sana kuokoa tani nyingi za misitu ambazo zinafyekwa na watu kwa maslahi yao

Alifafanua kuwa mpango huo wa MKUHUMI ni muhimu sana kwa maendeleo ya Nchi hivyo kinachoitajika kwa sasa ni suala zima la uhamasishaji baina ya watendaji wa mpango huo pamoja na wananchi ambao wakati mwingine wanaharibu misitu bila kujua umuhimu wake.

“huu mpango ni muhimu sana na kwa hali hiyo  napenda kuwasihi wananchi waupokee kwa kuwa una manufaa sana na kama utatumika vema utaweza kuhamisisha suala zima la upandaji wa miti  pamoja na misitu ambayo kwa sasa kwenye baadhi ya maeneo misitu hakuna huku hata iliyopo wakati mwingine inafyekwa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache”aliongeza Nyirembe

Katika hatua nyingine Mratibu wa mradi  huo wa MKUHUMI wilaya ya Kilosa,Hassani Chikira alisema kuwa mpango huo ni muhimu sana kwa Nchi ya Tanzania hususani kwenye suala la Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa kuwa unawahimiza wananchi walime na kuhifadhi Misitu ili waweze kupata fedha mbalimbali ambazo zinatumika kwa ajili ya masuala mengine ya kijamii

Akielezea mradi huo hapa nchini kwa sasa alisema kuwa umeshafanyiwa  uhamasishaji katika kanda  mbili ambapo viijiji kumi na nane kutoka kanda ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Manyara,Singida,na Dodoma, huku kwa upande wa kanda ya Mashariki ikiwa ni mikoa ya Pwani,Morogoro,na Dar es saalam

Aliongeza kuwa Wilaya ambazo nazo zimefanikiwa kufikiwa na mradi huo ndani ya kanda hizo mbili ni wilaya ya Babati pamoja na Wilaya ya Kongwa huku mpaka sasa mafanikio ya mpango huo yakiwa yameanza kuonekana  hali ambayo nayo itachangia sana kupunguza tatizo la uharibifu wa misitu.

MWISHO

No comments:

Post a Comment