Sunday, November 11, 2012

MKUU WA WILAYA AAGIZA VIONGOZI KUPANDA MITI

 MKUU WA WILAYA YA HAI,NOVATUS MAKUNGA

MKUU WA WILAYA AAGIZA VIONGOZI KUPANDA MITI

NA MWANDISHI WETU HAI


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kutoa tuzo kwa watu wanaopanda miti ili kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Brigedia Jenerali Kayombo aliyasema hayo juzi mji mdogo wa Mirerani kwenye mdahalo wa mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kupunguza athari zake uliondaliwa na mtandao wa asasi za kijamii mkoani humo Macsnet na The Foundation for Civil Society.
Alisema ili kuhakikisha jamii inapenda kutunza mazingira kwa kupanda miti uongozi wa wilaya hiyo unatakiwa kujipanga kutoa tuzo kwa washindi wa upandaji miti ili kuongeza hamasa ya kutunza mazingira wilayani humo.
Alisema mabadiliko ya tabia nchi ni suala ambalo hivi sasa linazungumzwa na wasomi,wanasayansi,wanasiasa na jamii kwa ujumla hivyo juhudi zinapaswa kufanyika ili kuhakikisha mabadiliko ya tabia nchi yanadhibitiwa.
“Juhudi za makusudi,elimu na sera ziendelee kutolewa kwa jamii kwani uelewa mdogo na dhamira ya wenye dhamana ni ya mashaka katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hivi sasa,” alisema Brigedia Jenerali Kayombo.
Mtoa mada Jackson Muro alisema madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ni ukame,magonjwa ya binadamu,mifugo,wanyama na mimea,mafuriko yasiyotegemewa,sunami  theluji kuyeyuka,kukosekana mvua na kina cha bahari au ziwa kupungua.

Alisema namna ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ni kutunza uoto wa asili,kupunguza uzalishaji wa hewa na gesi,kupanda miti ili inyonye hewa ukaa inayopanda angani na kuchanganya mazao ya kawaida na misitu.

“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la chakula duniani FAO mwaka 2005 ulionyesha kiwango cha ukataji misitu duniani umefikia hekta milioni 7.3 milioni kwa mwaka hivyo hewa ya ukaa kushindwa kufyozwa,” alisema Muro.

Naye,mmoja kati ya washiriki wa mdahalo huo,Kaanael Minja alimuuliza mkuu huyo wa wilaya nani anatoa kibali cha kukatwa mkaa wilayani humo kwani hivi sasa uuzwaji wa mkaa umeenea na hakuna hatua inayochukuliwa.
Hata hivyo,Brigedia Jenerali Kayombo alisema hakuna kibali kinachotolewa na mtu cha kukata mkaa kwenye wilaya hiyo,hivyo ushirikiano baina ya viongozi na jamii uongezwe ili kukomesha hali hiyo kwani kijiografia Simanjiro ni kubwa. 

MWENYEKITI WA KIJIJI MONDULI,JIMBONI KWA LOWASA ANUSURIKA KIPIGO KITAKATIFU



Joseph Ngilisho,Arusha
 
MWENYEKITI wa kijiji cha Losirwa kata ya Esilalei wilayani Monduli,  George Arpakwa anatuhumiwa na wananchi wake kujihusisha na ufisadi wa uuzaji wa ardhi ya kijiji kiholela hali inayokwamisha shughuli za maendeleo  kijiji hapo.
 
Wananchi hao wakizungumza kwa masikitiko makubwa katika mkutano wa hadhara kijiji hapo wamedai kuwa wamechoshwa na uongozi wa mwenyekiti huyo kwa kushindwa kuonyesha uwadilifu wake kwa jamiii badala yake amegeukia maeneo ya kijiji ambayo amekuwa akiyauza kinyume na sheria.
 
Mwenyekiti huyo ambaye alinusulika kipigo cha wananchi wake waliokuwa na jazba katika mkutano huo,aliamua kuvunja mkutano huo ghafla baada ya kubaini kwamba miongoni mwa waliohudhulia mkutano huo walikuwemo waandishi wa habari.
 
‘’huu mkutano ni wa kijiji waandishi wa habari hawaruhusiwi kuhudhuria hapa ‘’alitamka maneno hayo huku akitokomea gizani na makablasha pasipo julikana.

Katika hali ya kushangaza mwenyekiti huyo aliamua kumkunja shati mmoja ya wazee wa ukoo Leigwanani aliyekuwa akiwatetea waandishi wa habari waendelee kuwepo katika mkutano huo kwa ajili ya kuijulisha jamii ,hali ambayo ilizua taflani kubwa kwa wananchi kutaka kumpiga mwenyekiti huyo.
 
Mmoja ya wanakijiji hao,Romeni ole Meiya alieleza kushangazwa na tukio la mwenyekiti huyo na kudai kuwa mkutano huo ni muhimu sana kwa kujua mustakabali wa maeneo yao ambayo huyatumia kwa ajili ya malisho ya mifugo yao kutokana na kuwepo dalili mbaya kwa kiongozi wao kucheza mchezo mchafu.
 
Alisema kuwa wameshangazwa kuona baadhi ya maeneo ya malisho na mapito ya mifugo pamoja na mabwawa kuwekewa uzio kuashiria kuwa mifugo hairuhusiwi kuingia eneo hilo licha ya maeneo hayo kutengwa kwa ajili ya kuhudumia mifugo yao.
 
Alisema hawana imani tena na mwenyekiti wao ambaye sasa ameonyesha udhaifu wake katika utendaji wake wa kazi  hivyo wanamtaka achie ngazi na kwasasa hawamtambui kama yeye nikiongozi wa jamii hiyo ya kifugaji .
 
Naye Kiteho  Richard alisema kuwa mwenyekiti wao ameonyesha dhahili udhaifu mkubwa alionao kwa kuogopa kufichuka kwa madhambi yake  baada ya kubaini kuwepo kwa waandishi wa habari,hata hivyo alisisitiza kuwa kijiji kimeamua kutomtambua tena na kunafanya mkakati wa kupata mwenyekiti wa muda.
 
‘’Kama mwenyekiti hahusiki na kuuza maeneo ya wananchi kwanini amekimbia mkutano hii inaonyesha kua anahusika kwa asilimia kubwa ndio mana alipowaona waandishi wa habari akakimbia akijua siri  inafichuka" Alisema Richard"
 
Wananchi hao waliandamana hadi ofisi ya mwenyekiti huyo nakuchukua jukumu kali la kuifunga ofisi hiyo wakiamini kuwa ninjia moja wapo ya kupata suluhisho la Ardhi yao kumilikiwa na wenye pesa wachache huku wakiomba serikali kushughulikia tatizo hilo likiwa bado halijaleta hadhari kubwa kwa jamii.
 
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Monduli ,Jowika Kasunga akizungumza kwa njia ya simu amekiri kupokea taarifa hizo za malalamiko ya wananchi nakuahidi kuwa anazifanyia kazi ilikubaini ukweli wa jambo hilo.
 
mwisho.
 

Friday, November 9, 2012

Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kucheki afya zao mara kwa mara

Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kucheki afya zao mara kwa mara


Na Anna Nkinda – Maelezo
…………………………………………
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameitaka jamii kujenga mazoea ya kujichunguza afya zao mara kwa mara ili kuepuka maradhi au vifo visivyo na lazima kwani hivi sasa kuna maradhi mbalimbali yanayotokana na mazingira na aina ya mtindo wa maisha  na hivyo kurudisha nyuma maendeleo  binafsi na taifa kwa ujumla.

 Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji huduma ya afya kwa jamii ikiwemo uchunguzi wa saratani iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salam.

 Mama Kikwete pia aliitaka jamii kubadilisha mtazamo juu ya afya ya uzazi na mtoto kuwa inamhusu mama peke yake bali kila mmoja katika familia anahusika  ingawa hapo awali wanaume walionekana kutengwa na kutowajibika ipasavyo hivyo kusababisha kuzorota kwa afya ya uzazi na mtoto.
  “Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na wadau wake hivi sasa wametuanzishia mchakato huu, awali huduma hii ilijulikana kama afya ya mama na mtoto lakini sasa inajulikana kama afya ya uzazi na mtoto hii ni kuonesha kwamba kila mmoja wetu ndani ya familia  anawajibika”, alisema Mama Kikwete.

CHAMA CHA KIJAMII CHATOA TAMKO DHIDI YA VIONGOZI WA KIISLAMU

Na Queen Lema,Arusha

CHAMA CHA KIJAMII CHATOA TAMKO DHIDI YA VIONGOZI WA KIISLAMU


CHAMA cha Kijamii  hapa nchini (CCK)kimeipinga kauli ya Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Shehe Ponda Isa Ponda ambayo ilikuwa inamtaka Raisi Kikwete atoe amri ya kuwafungulia waislamu wote walioshikiliwa na jeshi la polisi kwa makosa ya kufanya maandamano bila kibali na kufanya uharibifu wa makanisa mbalimbali Jijini Dar es salaam

Akiongea na waandishi wa habari mapema jana mjini hapa Katibu mkuu wa chama hicho Bw Renatus Muabhi alisema kuwa kauli hiyo ni kauli ya uchochezi na uharibifu wa amani hasa kwa mkoa wa Dar es  salaam ambapo mpaka sasa madhara mbalimbali yameshatokea

Alisema kuwa Kiongozi huyo wa dini ya kiislamu hakutoa kauli nzuri kwani kauli hiyo imechangia sana baadhi ya waumini wa dini hiyo kupata vichwa na kufanya vurugu huku kama angeweza kutumia vema nafasi yake aliyonayo katika jamii basi angeweza kurudisha amani hata kwa kiwango kidogo sana .

Aliongeza kuwa viongozi hao wa dini wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia vema nafasi yao katika kuleta amani na badala yake wasitoe matamko mbalimbali ambayo ndiyo yanayofanya na kusababisha uvunjifu wa amani kwa ajili ya itikadi mbalimbali na za watu tofautitofauti.

“Hivi karibuni Raisi Kikwete alitoa Tamko ambalo lilikuwa linaani matukio yalifanywa na baadhi ya watu lakini baada ya muda huyu kiongozi naye akatoa tamko lake ambalo lilifanya uchochezi mkubwa sana kwa waumini sasa anapaswa kujua na kutamnbua kuwa anatakiwa kutumia vema nafasi yake katika jamii kwani kama kiongozi wa dini hakupaswa kutoa tamko la kumuonya Raisi wa Nchi  na badala yake angetumia vema busara kwa jambo hilo “alisema

Pia alisema kuwa Naye Raisi wa kikwete kuhakikisha kuwa anawachukulia hatua wote waliohusika na kuamini kuwa yeye ndiye suluhisho la masuala kama hayo ambayo yanafanya amani ya nchi ya Tanzania kuweza kupotea kwa vyanzo vidogo vidogo.

Katika hatua nyingine alibainisha kuwa pamoja na kuwa CCK kinalaani sana matukio kama hayo lakini nayo Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa inawachukulia hatua kali na za kisheria  kwa wale wote ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine katika kuvuruga amani ya Nchi hivi karibuni kutokana na Matukio ya itikadi za Kidini

Bw Renatus alifafanua kuwa endapo kama Serikali haitaweza kufanya hivyo basi amani ya Nchi ya Tanzania itayumba huku hali hiyo ikisababisha sana kuwepo kwa mdodoro mkubwa wa uchumi hasa kwa watu wa vipato vya chini kwa kuwa hawataweza kufanya kazi zao sanjari kukithiri kwa vifo ambavyo si vya lazima.

“Kwa  mfano kama juzi kumetokea vurugu kubwa sana hasa maeneo ya Kariakoo ambapo ndipo eneo la Uchumi mkubwa sana hasa kwa watu wa Dar  na walionekana kuathirika sana ni kina mama pamoja na watoto sasa kama hali nhii itaendelea hivi ni wazi kuwa tutakuwa tunaruhusu umaskini, lakini kama viongozi wa Dini watasimama na Serikali itawachukulia hatua basi haya matukio yatakuwa ni historia kubwa sana kwa jamii “aliongeza bw Renatus

Awali Bw Renatus alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kuwa na Utii wa sheria pamoja na mamlaka ambazo zipo ndani ya nchi hasa vyombo vya dola kuwa ni wajibu wao kutambua kuwa jamii inaweza kuwa ni sehemu kubwa sana ya machafuko ya nchi kwa kufuatafuata mkumbo hasa kutoka kwa viongozi wa Kidini na Kisiasa kwa malengo ambayo hayajulikani,hivyo wasikubali kutumika kama kuni ili kuepusha madhara hasa kwa wananchi wa vipato vya chini.

MWISHO

ELIMU YA MAZINGIRA IANZIE KUANZIA NGAZI YA CHEKECHEA ILI KUOKOA JAMII DHIDI YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

ELIMU YA MAZINGIRA IANZIE KUANZIA NGAZI YA CHEKECHEA ILI KUOKOA JAMII DHIDI YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Na MWANDISHI WETU, ARUSHA

IMEELEZWA kuwa endapo kama wanafunzi kuanzia ngazi ya madarasa ya awaali watafundishwa na kupewa mbinu za kutunza mazingira yanayowazunguka  basi wanafunzi hao watakuwa ni  wataalamu wazuri wa kutunza na kuthamini mazingira tofauti na sasa ambapo bado wapo baadhi ya wananchi wa maeneo mbalimbali ambao wanaharibu vibaya vyanzo vya mazingira kwa kushirikiana na watoto wao kwa kuwa hawana elimu ya kutosha huku watoto hao wakiona kuwa uharibifu wa mazingira ni jambo la  kawaida sana.

Wito huo umetolewa mjini Arusha na Mratibu wa shirika la Roots and Shoots,Bw Japhet Mwanangombe mapema wiki hii wakati akiongea na wanafunzi ambao ni wadau  wa mazingira (waelimishaji rika) zaidi ya 190 kutoka katika shule mbalimbali za msingi na Sekondari  kwa mkoa wa Arusha

Bw Mwanangombe alisema kuwa  kwa sasa  ni vema kama somo la elimu ya mazingira likafanywa kama somo lenye umuhimu mkubwa sana kwa wanafunzi kuanzia wale wa madarasa ya awali  kwa kuwa kama wanafunzi hao wataweza kupata vema elimu hiyo basi watakuwa ni mabalozi wazuri sana wa mazingira tofauti na sasa ambapo kwa  somo hilo linatolewa na wadau mbalimbali huku hata baadhi ya wazazi na wakuu wa shule wakiona kuwa ni moja ya elimu ambayo haina tija sana kwenye Jamii

Alisema kuwa elimu hiyo inapoanzia kuanzia ngazi ya chini kabisa itaweza kuwafanya watoto hata kuweza kuyapenda na kuyathamini mazingira ya Nchi na hivyo kukemea vikali sana suala zima la uharibifu wa mazingira ambapo mara nyingine unafanywa na wazazi au walezi wao kwa kuwa hawana elimu ya kutosha juu ya madhara ya uharibifu  huo.

“tuseme tusemavyo tuende tuendako  hii elimu ni ya muhimu sana kwenye Nchi yetu tena hususani Vijijini lakini kama tutakuwa tunaendelea kusema kuwa tuyapende mazingira huku hiki kizazi kikiwa hakiambiwi madhara ya uharibifu bado hatusaidii Jamii ila hawa watoto wetu wanatakiwa wapewe elimu hii ili kama hata wazazi wao  hawana elimu ya kutosha basi watawafundisha  wazazi wao  na hapo mazingira yataweza kuhifadhika tena hasa yale ya Vijijini,Aliongeza Bw Mwanangombe.

Mbali na hayo Mratibu huyo alisema kuwa nao wakuu wa shule wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatoa vipaumbele sanjari na uanzishwaji wa vitalu vya miti ndani ya shule zao na kuachana na tabia ya kuwakataza baadhi ya wanafunzi ambao wanamsukumo na suala zima la mazingira kwani kwa hali hiyo wanachangia sana uharibifu wa mazingira ambapo madhara kwa sasa yametanda sana ndani ya uso wa dunia.

Aliwataka wadau hao wa elimu ambao ni wakuu wa shule kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa hata na mashindano ya kimazingira ambayo yataweza kuwapa wanafunzi fursa ya kuyapenda na kuthamini mazingira hasa kwa njia ya upandaji wa miti hali ambayo nayo itafanya jamii kuepukana na ukame ambao kwa sasa upo kwenye baadhi ya vijiji  na kutokana na ukame huo unasababisha hata vifo vya wanyama na mimea kukauka.

Nao wanafunzi hao walisema kuwa pamoja na kuwa Shirika hilo linawawezesha katika masuala mbalimbali hasa ya utunzaji wa mazingira basi jamii nayo hasa kupitia kwenye Familia zao na Serikali za mitaa zinatakiwa kuwapokea na kuacha tabia ya kuwadharau kutokana na kuwa na umri mdogo kwani kupitia kwao wanaweza kufanya mabadiliko makubwa sana katika sekta hiyo ya mazingira.

MWISHO.



HALMASHAURI YA ARUSHA VIJIJINI INAKABILIWA NA UHABA WA MAPATO

Na  MWANDISHI WETU


HALMASHAURI YA ARUSHA VIJIJINI INAKABILIWA NA UHABA WA MAPATO

HALMASHAURI ya Arusha Vijijini Mkoani hapa inakabiliwa na uhaba wa mapato kutokana na baadhi ya watendaji wa halamshauri hiyo kushindwa kufuatilia kwa undani sana baadhi ya vyanzo vya mapato hali ambayo kama haitaweza kutatuliwa kwa haraka sana basi itasababisha madhara makubwa hasa kwenye malengo ya halmashauri hiyo kwenye jamii

Hayo yamebainishwa Wilayani humo na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo bw Khalifa Idda mapema juzi wakati akiongea katika baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo baraza hilo pia liliwashirikisha wananchi wa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Bw Idda alisema kuwa kwa sasa bado kuna upungufu mkubwa sana wa  mapato ya kutosha katika halmashauri hiyo ingawaje ina vyanzo vingi sana vya mapato hali amnbayo inasababisha kuonekane taa ya hatari hususani katika shuguli za maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo

Aliongeza kuwa ingawaje wilaya hiyo ina vyanzo vingi sana vya mapato bado kuna uitaji mkubwa sana wa watendaji wa halamshauri hiyo kuhakikisha kuwa wanaongeza nguvu zaidi katika kusaka na kubuni aina mpya ya vyanzo sanjari na kuhakikisha kuwa vyanzo ambavyo vipo vinatoa mapato kwa mujibu wa sheria na kanuni za Halmashauri hiyo

‘tuna upungufu mkubwa sana wa masuala ya fedha ndani ya halmashauri yetu nah ii ni kutokana na kuwa  na mapato madogo katika vyanzo vyetu  na hili suala kwa kweli halitupendezi kabisa kwani kama hali itaendelea hivi ni wazi kuwa hata ,mipango yetu kwa wananchi itakwama sana na tutasababisha madhara makubwa sana’aliongeza Bw Idda

Pia alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya uhaba wa mapato kutoka kwenye vyanzo vya kudumu vya Halmashauri hiyo wantarajia kuhakikisha kuwa kila mkuu wa Idara anatumia vema taaluma yake huku akifuatilia kwa ukaribu sana vyanzo vyote kwani kama watafanya hivyo basi watachangia kwa kiwango kikubwa sana maendeleo ya mapato

Hataivyo alifafanua kuwa mara baada ya kukaa chini na wakuu wa idara pamoja na wachumi wa halmashauri hiyo hivi karibuni wataweza kuweka kipaumbele kikubwa sana na kuhakikisha kuwa wanabuni vyanzo vipya na kuimarisha vile vya zamani ambapo kama mtendaji wa halmashauri hiyo hataweza kufanya kazi yake kikamilifu basi watachukuliwa hatua kali na za kisheria.

Katika hatua nyingine madiwani wa baraza hilo walisema kuwa suala hilo la uhaba wa vyanzo vya mapato sio suala dogo kabisa kwani linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuweza kunusuru Halmashauri hiyo dhidi ya Majanga mbalimbali ingawaje nao wakuu wa idara nao wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa haraka sana.

Madiwani hao walisema kuwa ni aibu kubwa sana kwa halmashauri hiyo kukosa mapato huku ikiwa na vyanzo vingi sana vya mapato na aibu hiyo inatakiwa kufutwa na wakuu wa idara hasa Mweka hazina wa Halmashauri ambapo wanatakiwa kutembea mitaani na kuangali hali ilivyo na kuachana na tabia ya kudai kuwa halmashauri haina fedha huku vyanzo vingine vikiwa vinateketea  na watendaji wasio wahaminifu

‘Mweka hazina hapaswi kukaa ofisini na kusubiria taarifa anatakiwa kutumia taaluma yake vema na kuanza kubuni vyanzo lakini sio hilo pekee bali anatakiwa pia hata kwenda kwenye vyanzo vya mapato na kama ataweza kutembelea vyanzo vya mapato kila mara hata watendaji wazembe watajulikana na wale wanaokula fedha za halmashauri kwa madai kuwa mapato hakuna basi na wao wataweza kujulikana na hapo tutarudisha vyanzo vyetu jamani tuache kukaa ofisini na kusubiri kudanganywa na baadhi ya watu “waliongeza madiwani hao

MWISHO

CHADEMA YADAKA VITONGOJI SITA KATI YA TISA NDANI YA MJI MDOGO WA USA RIVER

CHADEMA YADAKA VITONGOJI SITA KATI YA TISA NDANI YA MJI MDOGO WA USA RIVER

Na Queen Lema, MERU

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo mkoani hapa kimefanikiwa kuibuka
mshindi wa  vitongoji sita kati ya tisa vya mji mdogo wa usariver
wilyani Meru na kuahidi kufanya mabadiliko makubwa sana katika nyanja
za uchumi wa Mji huo

Akiongea na Majira mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya vitongoji
vyote katibu wa Chadema mkoa wa Arusha bw Amani Golugwa alisema kuwa
ushindi huo umetokana na mabadiliko mbalimbaliu ambayo yanafanywa na
chama hicho sanajari na kutoa Muongozo imara kwa maisha ya Mtanzania
hasa wa Eneo hilo la Usa River

Bw Golugwa aliongeza kuwa pamoja na kuwa wamefanikiwa kupata ushindi
kwa Vitongoji kama sita bado watafanya mabadiliko makubwa sana katika
Mji huo wa Usa River ambapo mabadiliko hayo ni pamoja na kukuza uchumi
wa mji huo katika halmashauri hiyo ambayo hapo awali palikuwa na
matatizo mbali mbali ya uchumi huku hali hiyo ikisababisha hata
umaskini mkubwa sana

‘leo tumeweza kupata Vitongoji kama sita huku vitatu tukivikosa na
sasa hii ni imara sana kwetu kwa kuwa sasa halamshauri itakuwa kama
ile ya Karatu kwa kuwa tutafanya mabadiliko makubwa sana na itafanya
kuchochea hata Umaskini kupoungua kwa kuwa tutaweza kuimarisha sana
mji huu mdogo wa Usa river na miji mingine nayo itaiga mfano mzuri wa
uongozi hasa katika nyanja za uchumi ambao unatekwa na baadhi ya
viongozi kwa manufaa yao wenyewe”aliongeza Bw Golugwa

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho bw Freeman
Mbowe alisema kuwa kupitia ushindi huo bado chama chake hasa kwa mkoa
wa Arusha kina nafasi kubwa sana ya kuweza kuboresha mabadiliko
makubwa sana ingawaje Vitongoji Vitatu vimechukuliwa na wapinzani wao.

“kushindwa kwa vitongoji vitatu sio sababu bali kutokana na hili sisi
tunaweza kusema kuwa huu ni ushindi imara na ushindi huu utaweza
kutufanya tuweze kuchapa kazi kwa kwenda mbele kwa hivyo tunaendelea
kupambana ma kuhakikisha kuwa tunafanya mabadiliko kulingana na chama
chetu:”aliongeza bw Mbowe

Hataivyo katika uchaguzi huo ambao ulishirikisha Vitongoji tisa
Chadema imechukua vitongoji vya Manyata
Kati,kisambare,Magadini,
Ngarasero, Nganana.Mji mwema    wakati kwa
upande wa  CCM wamechukua Vitongoji vya Magadirisho,Usa
madukani,pamoja na Mlima Sioni

MWISHO

SERIKALI YA TANZANIA YAHIDI KUBORESHA SEKTA YA AFYA


Na Joseph Ngilisho,ARUSHA

RAIS  Jakaya Kikwete amesema kuwa serikali ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha vituo vya afya na zahanati hapa nchini vinajengwa kwenye vijiji, kata ,wilaya na kwamba hospitali za mkoa zinakuwa na hadhi ya rufaa.

Rais Kikwete ameyasema hayol eo wakati akizindua hospitali teule ya Olturumenti kuwa ya wilaya, ambapo hapo awali ilikuwa kituo cha Afya katika halimashauri ya wilaya ya Arusha,na kutoa wito kwa vituo vya afya na zahanati zilizopo kuboreshwa ili ziwe na hadhi ya kulaza wagonjwa.

Aidha alisema utekelezaji wa mpango wa mpango huo umeanza na  unalengo la kuwasogezea  huduma za Afya  wananchi kwa ukaribu na kuondokana na  adha inayowakabili ya kufuata huduma hiyo umbali mrefu .

Alisema katika kukamilisha mpango huo serikali imeongeza mara sita bajeti yake kutoka shilingi bilioni 271 ya mwaka 2005 na kufikia kiasi cha shilingi Trioni 6.2 ,ambapo lengo ni kuhakikisha kuna kuwepo na vituo vya Afya na zahanati za kutosha hapa nchini.

Hata hivyo aliwataka viongozi husika akiwemo waziri wan chi ofisi ya rais dkt Hawa Ghasia kuzifanyia kazi changamoto zote zinazozikabili hospitali vituo vya Afya na zahanati ili kuhakikisha vinatoa huduma iliyo bora itakayo saidia kupunguza kero kwa wananchi.

Kikwete aliongeza kwa kusema kuwa serikali imefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na maambukizi ya malaria kutoka asilimia 14 na kufikia asilimia 2 ,sanjari na kuweka mipango mikakati mbalimbali ambayo inalenga kuimarisha zaidi afya ya Mtanzania dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo
 
Alitaja Mikakati hiyo ambayo inaendelea kutekelezwa ili kuepusha jamii na maambukiz mapya ya ugonjwa wa Malaria kuwa ni pamoja na kugawa vyandaru viwili  kwa kaya,ambapo hadi sasa  Jumla ya Vyandarua Milioni 13 vimeshagawiwa,huku mkakati mwingine ambao unafuatwa ni kupuliza dawa kwa kila kaya,na mkakati mwingine  ni kujenga na kuimarisha zaidi kiwanda ambacho kinazalisha Viluilui ambao wataweza kushambulia wadudu wa Malaria.

Awali mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Arusha Thobias Mkina alisema kuwa pamoja na kuwa Ujenzi wa hospitali hiyo ya Oltument umegarimu kiasi cha  zaidi ya Milioni 924 lakini bado kuna changamoto lukuki ndani ya Hospitali hiyo ambayo inatarajia kuhudumia maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo na nyingine za jirani.

Dkt Thobias alitaja changamoto kubwa sana ndani ya hospitali hiyo kuwa wa majengo ya kutosha hasa wadi za wamama wajawazito, watoto , chumba cha X ray, pamoja chumba cha kupimia magonjwa ya VVU hali ambayo inatakiwa kuangaliwa kwa haraka sana ili kuweza kuboresha afya za wananchi wa wilaya hiyo

MBOWE ASEMA KUWA YUPO TAYARI KUACHA CHADEMA KAMA HAKITAANGALIA MAHITAJI MUHIMU YA MAISHA YA MTANZANIA

MBOWE ASEMA KUWA YUPO TAYARI KUACHA CHADEMA KAMA HAKITAANGALIA
MAHITAJI MUHIMU YA MAISHA YA MTANZANIA


Na Queen Lema, MERU

MWENYEKITI  wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA)Bw Freeman
Mbowe amesema kuwa yupo  tayari kuacha chama chake endapo kama chama
hicho  hakitaweza kufuata sheria taratibu na kanuni za maisha bora kwa
mtanzania kwa kuwa kwa sasa wapo baadhi ya watu ambao wamefunga ndoa
na vyama vya siasa hali ambayo inasababisha hata shuguli za maendeleo
kukwama

Bw Mbowe aliyasema hayo wilayani Meru mkoani hapa  katika harambee ya
shule ya ufundi ya Olokii iliyo chini ya kanisa la Kiinjili la
kilutheri dayosisi ya kaskazini kati, wakati alipokuwa mgeni rasmi
mapema jana

Bw Mbowe alisema kuwa endapo kama chama chake hakitaweza kutumia vema
nafasi yake katika kutetea haki za mtanzania hususani katika sekta ya
elimu basi ni bora kuachia ngazi kwa kuwa chama cha siasa sio baba
wala mama bali ni mpango wa kupingana kwa hoja ingawaje kwa sasa wapo
baadhi ya watu ambao wamefunga ndoa na vyama vya siasa na kusababisha
hata kukitihiri kwa mgawanyo mkubwa sana ndani ya Jamii

“utakuta mtu akiona kuwa eti Mbowe yupo kanisani na anafanya harambee
haingii kwa kuwa ni Chadema nay eye ni CCM sasa hali itaenda mpaka
lini wakati Chadema ni mali ya wananchi na CCM pia ni mali ya wananchi
na kutokana na hali kama hii ndiyo inayochangia sana hata baadhi ya
watu wanashindwa kufuata sheria na kanuni za maisha bora kwa mtanzania
na wengine wanateseka kiasi cha kufa sasa mimi sijafunga ndoa na
Chadema kwa kuwa sio baba yangu wala Mama yangu’aliongeza bw Mbowe

Katika hatua nyingine alisema kuwa bado anailaumu sana Serikali ya
sasa kwa kushindwa kutekeleza sera ya elimu na kusababisha hata elimu
ya Tanzania kuwa hafifu tofauti na nchi nyingine ambazo zinaendelea
huku kundi kubwa sana la wanafunzi  wakiwa bado wanaendelea kuzorota
Mitaani hili hali Serikali inauwezo mkubwa sana wa kuwasomesha
kutokana na Rasilimali ambazo zipo.

Aliongeza kuwa kundi kubwa sana la vijana ambalo linaachwa mitaani
hasa wale ambao wamekosa nafasi kwa darasa la Saba,kidato cha Nne,
kidato cha Sita ndio wanaosababisha hata umaskini kukitihiri kwa kuwa
baadhi yao wanakosa mahitaji muhimu huku kwa nchi zilizoendelea vijana
kama hao wanapewa kipaumbele kwa kuhakikisha kuwa wanapata fursa
mbalimbali za elimu na ajira imara.

‘Sasa hivi unakuta baadhi ya watu eti wanaawacha hawa wanafunzi ambao
wameitimu madaraja mbalimbali alafu nchi inadai kuwa inapambana na
Umaskini sasa kama sio uongo ni nini utapambana na umaskini ilihali
watu hawana elimu na ndio maana Nchi jirani yetu ya Kenya inatuzidi na
idadi ya watoto wa vigogo wanaosoma Kenya na Uganda ni kubwa kuliko
ile ya watoto wa vigogo kutoka katika nchi hizo wanaokuja Tanzania
kusoma tuamke watanzania na tuangalie hili kwa undani sana’aliongeza
Mboye.

Awali Askofu wa kanisa la kiinjili la kilutheri mkoani hapa(
KKKT)dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt Thomas Laizer alisema kuwa ni
jambo la ajabu sana kwa wanasiasa kuchukiana ovyo kwa kuwa siasa
inaenda kama mchezo wa mpira ambao kamwe hautabiriki na hivyo
wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanajijengea tabia ya kupenda na
kuthaminiana wao kwa wao hasa kwenye majukumu ya msingi ya
Kimaendeleo.

Dkt Thomas alisema kuwa wapinzani kuwakataa watawala na watawala
kuwakataa wapinzani si jambo jema na halitakiwi kuendelezwa kwa sasa
kwani wote wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakuwa kitu kimoja na kutatua
matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili jamii kwa  sasa likiwemo suala
zima la uvunjifu wa amani ndani ya Nchi.

“leo mtu wa CCM hampendi huyu wa Chadema ambaye ni mpinzani wake
wakati kesho 2015 bado haujajua na kutambua kuwa atakayeongoza nchi
atakuwa ni ninani je akiwa ni Chadema ndiye kiongozi itakuwaje hivi
vyama vinatakiwa kufikiria na wanatakiwa kuwa na umoja na wala sio
kulumbana kwa vitu ambavyo havina maana kabisa shuguli za maendeleo
zipo nyingi sana na huo muda unaopotea bure utumike hasa kwenye
shuguli kama zetu za maendeleo ya jamii’aliongeza Dkt Laizer

Katika Harambee hiyo ambayo ni kwa ajili ya Mabweni ya wanafunzi wa
Shule hiyo ya ufundi ya Olokii zaidi ya Milioni kumi zilipatikana
ambapo iliongozwa na Bw Mbowe pamoja na wadau wengine wa elimu hapa
nchini.

MWISHO

Thursday, November 1, 2012