Diwani wa kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara,Justin Nyari akikagua nyumba ya mkazi wa mtaa wa
Songambele,Katarina Selemani iliyoanguka kutokana na mafuriko yaliyotokea juzi
na kuathiri baadhi ya nyumba na mazao ya wakazi wa kata hiyo.picha na Queen Lema,Simanjiro
Kamati ya maendeleo ya Kata ya Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, imetembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko
yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa sehemu tofauti hapa
nchini.
Akiongoza msafara huo juzi,Diwani wa kata ya Mirerani
Justin Nyari aliwapa pole waathirika wa mafuriko hayo ambapo nyumba zaidi ya 26
na mazao mbalimbali yaliathirika kutokana na mafuriko hayo.
Akizungumza na baadhi ya waathirika hao,Nyari alisema
ameshatoa taarifa kwa Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Simanjiro,Patrice Saduka kwa ajili ya hatua zaidi ya kutatua tatizo hilo.
“Hatua ya kwanza tuliyochukua na WDC yangu ni
kutembelea na kubaini sehemu zilizoathirika na kutoa taarifa wilayani na
watamtuma mhandisi Agai,lakini kubwa zaidi mji wa Mirerani unapaswa upimwe,”
alisema Nyari.
Hata hivyo,Diwani wa kata hiyo Nyari alimkabidhi
kifuta machozi cha fedha mmoja kati ya waathirika wa mafuriko hayo,Katarina
Selemani mkazi wa Songambele ambaye nyumba aliyokuwa anashi ilibomolewa na
mafuriko hayo.
Naye,mwathirika mwingine wa mafuriko hayo Boniface
Mboya,akizungumza mbele ya kamati hiyo alisema mafuriko hayo yameathiri eneo
analoishi kwani miti 750 ilichukuliwa na mafuriko,miche 1,300 na maua 250 na choo
kubomoka.
Baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo walidai
kuwa,mvua kubwa zilizonyesha kwenye maeneo tofauti ya mkoa wa
Arusha,yamesababisha mafuriko hayo yaliyopitia Msitu wa Mbogo,Mbuguni hadi eneo
hilo na
kuelekea Majengo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment