Na Gladness Mushi,Arusha
Jeshi la polisi Mkoani Manyara linamshikilia mfanyabiashara wa madini
ya Tanzanite,Lawi Abayo (33) kwa kudaiwa kumuua kwa kumpiga risasi
askari polisi wa kituo cha Mirerani Wilayani Simanjiro G.7037 Joseph
Tairo (28).
Akithibitisha kushikiliwa kwa mfanyabiashara huyo,Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Manyara,Kamishna Msaidizi Akili Mpwapwa alisema jana kuwa
Abayo alijisalimisha juzi kwenye kituo cha polisi wilayani Babati.
Kamanda Mpwapwa alisema baada ya mfanyabiashara huyo kujisalimisha
mwenyewe hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya
kumfikisha mtuhumiwa huyo Mahakamani ili kujibu shtaka la mauaji.
Hata hivyo,Kamanda Mpwapwa alithibitisha kushikiliwa kwa bastola
inayodaiwa kutumiwa na mfanyabiashara huyo kumuua Tairo na pia
wanalishikilia gari aina ya Prado alilotumia kutorokea mara baada ya
tukio hilo.
Askari huyo PC Tairo alifariki dunia Aprili 15 mwaka huu,kwenye
hospitali ya Muhimbili (Moi) baada ya kupigwa risasi ya kichwa na
kujeruhiwa Aprili 7 akiwa kazini mjini Mirerani na kuzikwa kijijini
kwao Kaboro,Mkuu Rombo Aprili 19.
Chanzo cha tukio hilo ni PC Tairo akiwa na askari mwenzake G.8523 PC
Martin,kumkamata mhalifu mmoja na wakati wakimpeleka kituoni ndipo
mfanyabiashara huyo akazuia zoezi hilo kwa kumpiga risasi askari huyo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment