Sunday, September 29, 2013

MUSWADA WA MAREKEBISHO YA KATIBA WATARAJIA KUKABIDHIWA KWA JK

MUSWADA wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, unatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete, wiki ijayo. Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vyake vilivyoko serikalini zimeeleza kuwa Rais Kikwete atakabidhiwa muswada huo mara atakaporejea nchini akitokea katika ziara yake ya nchi za Marekani na Canada.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, jana alilieleza gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuwa Muswada huo utawasilishwa kwa Rais Kikwete na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, baada ya kuuandaa vizuri na rais atauperuzi kabla ya kufikia uamuzi wa kuusaini au kutousaini.

Taarifa hizi zimepatikana siku chache baada ya kusambaa kwa tetesi zinazoeleza kuwa Rais Kikwete alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na baadhi ya maofisa walio katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujadili baadhi ya vipengele vilivyo kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambavyo vimeibua mvutano.

Hata hivyo, Jaji Werema aliliambia gazeti hili kuwa hana taarifa ni lini Dk. Kashilillah ataupeleka muswada huo Ikulu na hata alipoulizwa kuhusu tetesi zilizosambaa miongoni mwa jamii kuwa Rais alikutana na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na wale wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujadili mwenendo na mwelekeo wa rasimu hiyo, alisema hafahamu chochote.

“Muswada ukishatoka bungeni, kama umepitishwa huo haumhusu tena Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anakuwa nao Katibu wa Bunge. Yeye sasa anakuwa na kazi ya kuuweka vizuri, akikamilisha anauchukua na kuupeleka Ikulu kwa Rais kwa ajili ya kusaini.

“Yeye Rais akishapewa naye anauangalia, ukimpendeza anausaini, vinginevyo hausaini anaurudisha. Sasa hivi sasa anao Katibu wa Bunge, jua kuwa anayejua kama umesaini au hapana ni yeye na rais tu, wengine wote tunasubiri taarifa ya Katibu wa Bunge. Hayo mengine ya ataupeleka kwa njia gani na lini siyajui,” alisema Jaji Werema.

Taarifa zilizopatikana kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, zimeeleza kuwa kuna wasiwasi umetanda iwapo Rais atasaini muswada kwa sababu Tume ya Jaji Warioba bado haijampelekea rasimu ya pili ya Katiba, ambayo ndiyo hutoa mwelekeo wa kuitishwa kwa Bunge la Katiba.

Mmoja wa maofisa wa juu wa wizara hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake, ameeleza kuwa mvutano ulioibuka baada ya Tume ya Jaji Warioba kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya unaweza kuchelewesha kutolewa kwa rasimu ya pili ambayo ni lazima Rais akabidhiwe na aipitie, ndiyo hatua ya kuitwa kwa Bunge itakapofuata.

Alisema, kwa sasa hali ni ya wasiwasi kwa sababu ipo hofu kuwa rais anaweza asisaini muswada huo, bali atakachofanya ni kuandika dokezo litakalokuwa na sababu za kutoweka sahihi yake kwenye muswada kisha ataurejesha kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya kuupeleka tena bungeni kujadiliwa.

“Na hii ni kwa sababu Bunge la Katiba haliwezi kuitishwa bila Tume ya Jaji Warioba kupeleka rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais, na yapo mashaka kuwa hatapeleka kwa sasa kutokana na mwenendo wa mambo ulivyo.

“Sasa Jaji Warioba asipopeleka rasimu ya pili ina maana hata Bunge la Katiba halitakuwepo,” alisema.

Katibu wa Bunge, Dk. Kashilillah jana hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana mara kadhaa alipopigiwa, lakini duru za habari kutoka Ofisi ya Bunge zimedokeza kuwa anatarajiwa kuuwasilisha muswada huo kwa Rais Kikwete siku ya Jumatano, Oktoba 2, 2013.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Dk. Kashilillah amekwishakamilisha maandalizi ya muswada na sasa anamsubiri rais arejee nchini ili amkabidhi.

Imeelezwa kuwa hatua ya Rais Kikwete ya kutosaini muswada huo utakuwa ni mtego kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioupitisha kwa sababu watalazimika kukubaliana na mabadiliko yanayoshinikizwa na makundi mbalimbali ya jamii, ambayo yanadai kuwepo kwa kasoro ndani ya muswada.

Mabingwa wa mambo ya kibunge ambao wamekuwa wakizungumza na gazeti kwa nyakati tofauti, huku wakisisitiza majina yao kuhifadhiwa kwa kile wanachoeleza kuwa suala la Rasimu ya Katiba sasa ni nyeti, wameeleza kuwa uamuzi wa Rais Kikwete ndio utakaowaongoza wabunge wa CCM wanachopaswa kufanya na iwapo watapingana nao, ipo hatari ya Bunge kuvunjwa.

Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Bunge, iwapo Rais Kikwete hatasaini muswada huo na kuurejesha bungeni na iwapo wabunge nao wataupitisha tena bila kuufanyia marekebisho, Rais atalivunja Bunge.

No comments:

Post a Comment