SERIKALI kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) imelifungia Gazeti la
MTANZANIA kwa muda wa siku 90 kupitia Tangazo la Serikali namba 332 la
tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kile inachodai kuwa limekuwa likiandika
habari za kichochezi. Sambamba na MTANZANIA, pia imelifungia gazeti la
MWANACHI kwa muda wa siku 14 kwa madai hayo hayo.
Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari MAELEZO, Assah Mwambene, kwa vyombo vya habari vichache
vilivyotumiwa wito wa kuwepo kwa mkutano baina yake na vyombo hivyo.
Taarifa
hiyo iliyotolewa na Mwambene, ilisambazwa pia katika mitandao ya
kijamii na ilieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kulionya
mara nyingi MTANZANIA kuacha kuandika habari za uchochezi lakini
halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti.
Ilizitaja
habari inazodai kuwa za uchochezi kuwa ni pamoja na iliyochapishwa
katika toleo namba 7262 la Machi 20 mwaka huu iliyokuwa na kichwa cha
habari kisemacho ‘URAIS WA DAMU,’ na makala ya uchambuzi iliyochapishwa
Juni 12 katika toleo namba 7344 iliyokuwa na kichwa cha maneno
‘MAPINDUZI HAYAEPUKIKI.’
Habari nyingine iliyolalamikiwa na
serikali ni iliyochapishwa Jumatano ya Septemba 18 mwaka 2013 katika
ukurasa wa mbele wa toleo namba 73414 iliyobebwa na kichwa kisemacho
‘SERIKALI YANUKA DAMU.’
Taarifa ya Mwambene inadai kuwa habari
hiyo ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia
kompyuta na kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.
Aidha,
taarifa hiyo inaeleza kuwa habari hiyo haikuwa na uthibitisho na
ililituhumu Jeshi la Polisi kuhusika na wahanga walioumizwa na watu
wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa
vibaya na pia kuishitumu serikali kwa ugoigoi katika kushughulikia
matukio yenye sura ya kigaidi.
Kwa upande wa Gazeti la MWANANCHI,
serikali imeeleza kuwa imechukua uamuzi wa kulifungia kwa sababu ya
kuandika habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani na
imetoa mfano wa habari iliyokuwa na kichwa kisemacho MISHAHARA MIPYA
SERIKALINI 2013 na nyingine iliyokuwa na kichwa kilichosomeka ‘WAISLAM
WASALI CHINI YA ULINZI MKALI.’
No comments:
Post a Comment