Na Bety Alex, ngorongoro
Wahifadhi, watafiti na wataalam kadhaa wako katika harakati za kumsaka
Nyati wa ajabu anayedaiwa kuwa na rangi ya maziwa, ambaye hivi
karibuni amekuwa akionekana katika mwambao wa bonde kuu la Ngorongoro
(Kreta), na kusababisha tafrani kubwa.
Kwa mujibu wa mtalaam wa ikolojia katika mamlaka hiyo Patrice Mattay,
uwepo wa nyati (mbogo) huyo wa aina yake hifadhini hapo kumeibua suala
jipya katika utafiti wa wanyama pori kwani hakujawahi kuwepo Nyati
mwenye rangi nyeupe popote duniani.
Kwa kawaida Wanyama wote aina ya nyati huwa na ngozi yenye rangi nyeusi.
Nyati huyo mweupe aligundulika kwa mara ya kwanza na maafisa wa polisi
wanaofanya kazi katika kituo cha polisi kilichopo ndani ya hifadhi
hiyo ambao wanasema mnyama huyo hupita katika maeneo ya kituo hicho
majira ya asubuhi akiwa miongoni mwa Mbogo wengine takribani 20.
Ngorongoro ina nyati wapatao 350.
“Ni kweli hata mimi binafsi nimemshuhudia Nyati huyo mweupe akikatiza
katika sehemu mbalimbali za hifadhi ya Ngorongoro majira ya asubuhi
akiwa katika kundi la mbogo wengine,” alisema Mkuu wa kituo cha
Ngorongoro Afisa wa Polisi JJ Paul.
Hadi sasa ni maaskari wanaofanya doria katika maeneo ya hifadhi hiyo,
hususan nyakati za asubuhi, ndio wanaothibitisha kwa kiwango kikubwa
kumuona Nyati huyo wa ajabu ambaye sasa anatarajiwa kuwa atakuwa
kivutio kipya cha utalii katika Tanzania nchi ambayo ndiyo pekee
duniani mnyama huyo atakuwa anapatikana.
Meneja wa Uhifadhi katika mamlaka ya Ngorongoro, Amiyo T. Amiyo
amesema tayari shirika lake limekwisha tuma askari wake kadhaa kumsaka
Nyati huyo wa ajabu ili kubaini eneo ambalo anapatikana kwa ajili ya
kuwezesha utafiti zaidi.
“Na kwa mtu yeyote mwenye kutuletea taarifa kuhusu Nyati huyo mweupe
zitakazotuwezesha kumpata mnyama huyo basi naye pia atazawadiwa
ipasavyo,” alisema Amiyo.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndiyo inayoongoza kwa kupata watalii
wengi nchini na kwa mujibu wa Afisa utalii wa shirika hilo, Asantaeli
Melita, zaidi ya wageni 585,000 hutembelea eneo hilo, na hasa Kreta,
kila mwaka. Tanzania kwa ujumla hupata watalii milioni moja kwa mwaka.
Idadi ya wanyamapori walioko Ngorongoro kwa sasa inafikia 300,000
wengi wao wakiwa ndani ya bonde lenyewe huku baadhi, na hasa twiga
wakiishi nje ya kreta.
Mbali na Mbogo wa jabu aliyegunduliwa hivi karibuni, eneo la
Ngorongoro pia lina maajabu mengine kadhaa, ukiwemo kilima cha mchanga
unaotembea bila kusambaratika, idadi kubwa ya Kakakuona, mnyama
anayedaiwa kuwa na uwezo wa kutabiri, pamoja na idadi kubwa ya wanyama
adimu kama Mbwa-mwitu na Faru.
No comments:
Post a Comment