Na GLADNESS MUSHI, Manyara
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara, Mohamed Omary Farah, amegawa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh600,000 kwa timu mbili za soka za Mrara FC na Waangwaray FC za kata ya Babati.
Akigawa vifaa
hivyo jana kwenye uwanja wa Mrara uliopo mjini Babati, Farah ambaye pia ni
Diwani wa kata ya Babati alisema lengo la kugawa vifaa hivyo ni kuhakikisha
sekta ya michezo inapiga hatua katika eneo hilo.
Alisema anatoa
msaada huo wa vifaa vya michezo kwa lengo la kuwaendeleza ambapo timu hizo
mbili zilipatiwa kila moja seti moja ya sare za michezo ikiwemo tisheti, bukta
na soksi pamoja na mpira mmoja.
Alisema kupitia
michezo vijana wataweza kujinufaisha kwani hivi sasa michezo ni ajira na pia
wataweza kujiweka pembeni na mambo mabaya ikiwemo tabia za uhuni na uvutaji dawa
za kulevya.
Alisema
atahakikisha anakuwa nao sambamba katika michezo kwenye kuwaunga mkono ili timu
hizo ziweze kufika madaraja ya juu na kuzileta timu kubwa kwenye mji huo wa
Babati.
Hata hivyo,
mwakilishi wa timu ya Mrara FC Gerald Romly akitoa shukrani kwa niaba ya timu
hizo alisema watatumia msaada huo wa vifaa vya michezo kwa kuzitumia ipasavyo
kwa ajili ya lengo la kufanikisha michezo.
Romly alimshukuru
Farah kwa kuwapa msaada huo wa michezo na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano
wake, kwani ameonyesha moyo na kujali michezo inayofanywa na vijana wa eneo
hilo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment