MUSWADA wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Katiba wa mwaka 2013
uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, unatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais
Jakaya Kikwete, wiki ijayo. Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka
vyanzo vyake vilivyoko serikalini zimeeleza kuwa Rais Kikwete
atakabidhiwa muswada huo mara atakaporejea nchini akitokea katika ziara
yake ya nchi za Marekani na Canada.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, jana alilieleza
gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuwa Muswada huo
utawasilishwa kwa Rais Kikwete na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashilillah, baada ya kuuandaa vizuri na rais atauperuzi kabla ya
kufikia uamuzi wa kuusaini au kutousaini.
Taarifa hizi
zimepatikana siku chache baada ya kusambaa kwa tetesi zinazoeleza kuwa
Rais Kikwete alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba na baadhi ya maofisa walio katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujadili baadhi ya vipengele vilivyo
kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambavyo vimeibua mvutano.
Hata
hivyo, Jaji Werema aliliambia gazeti hili kuwa hana taarifa ni lini Dk.
Kashilillah ataupeleka muswada huo Ikulu na hata alipoulizwa kuhusu
tetesi zilizosambaa miongoni mwa jamii kuwa Rais alikutana na baadhi ya
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na wale wa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujadili mwenendo na mwelekeo wa rasimu
hiyo, alisema hafahamu chochote.
“Muswada ukishatoka bungeni,
kama umepitishwa huo haumhusu tena Waziri au Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, anakuwa nao Katibu wa Bunge. Yeye sasa anakuwa na kazi ya
kuuweka vizuri, akikamilisha anauchukua na kuupeleka Ikulu kwa Rais kwa
ajili ya kusaini.
“Yeye Rais akishapewa naye anauangalia,
ukimpendeza anausaini, vinginevyo hausaini anaurudisha. Sasa hivi sasa
anao Katibu wa Bunge, jua kuwa anayejua kama umesaini au hapana ni yeye
na rais tu, wengine wote tunasubiri taarifa ya Katibu wa Bunge. Hayo
mengine ya ataupeleka kwa njia gani na lini siyajui,” alisema Jaji
Werema.
Taarifa zilizopatikana kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,
zimeeleza kuwa kuna wasiwasi umetanda iwapo Rais atasaini muswada kwa
sababu Tume ya Jaji Warioba bado haijampelekea rasimu ya pili ya Katiba,
ambayo ndiyo hutoa mwelekeo wa kuitishwa kwa Bunge la Katiba.
Mmoja
wa maofisa wa juu wa wizara hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa
sharti la kutotajwa jina lake, ameeleza kuwa mvutano ulioibuka baada ya
Tume ya Jaji Warioba kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya unaweza
kuchelewesha kutolewa kwa rasimu ya pili ambayo ni lazima Rais
akabidhiwe na aipitie, ndiyo hatua ya kuitwa kwa Bunge itakapofuata.
Alisema,
kwa sasa hali ni ya wasiwasi kwa sababu ipo hofu kuwa rais anaweza
asisaini muswada huo, bali atakachofanya ni kuandika dokezo litakalokuwa
na sababu za kutoweka sahihi yake kwenye muswada kisha ataurejesha kwa
Katibu wa Bunge kwa ajili ya kuupeleka tena bungeni kujadiliwa.
“Na
hii ni kwa sababu Bunge la Katiba haliwezi kuitishwa bila Tume ya Jaji
Warioba kupeleka rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais, na yapo mashaka kuwa
hatapeleka kwa sasa kutokana na mwenendo wa mambo ulivyo.
“Sasa Jaji Warioba asipopeleka rasimu ya pili ina maana hata Bunge la Katiba halitakuwepo,” alisema.
Katibu
wa Bunge, Dk. Kashilillah jana hakuweza kupatikana kuzungumzia suala
hilo, baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana mara kadhaa
alipopigiwa, lakini duru za habari kutoka Ofisi ya Bunge zimedokeza kuwa
anatarajiwa kuuwasilisha muswada huo kwa Rais Kikwete siku ya Jumatano,
Oktoba 2, 2013.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Dk. Kashilillah
amekwishakamilisha maandalizi ya muswada na sasa anamsubiri rais arejee
nchini ili amkabidhi.
Imeelezwa kuwa hatua ya Rais Kikwete ya
kutosaini muswada huo utakuwa ni mtego kwa wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) walioupitisha kwa sababu watalazimika kukubaliana na
mabadiliko yanayoshinikizwa na makundi mbalimbali ya jamii, ambayo
yanadai kuwepo kwa kasoro ndani ya muswada.
Mabingwa wa mambo ya
kibunge ambao wamekuwa wakizungumza na gazeti kwa nyakati tofauti, huku
wakisisitiza majina yao kuhifadhiwa kwa kile wanachoeleza kuwa suala la
Rasimu ya Katiba sasa ni nyeti, wameeleza kuwa uamuzi wa Rais Kikwete
ndio utakaowaongoza wabunge wa CCM wanachopaswa kufanya na iwapo
watapingana nao, ipo hatari ya Bunge kuvunjwa.
Kwa mujibu wa
kanuni na taratibu za Bunge, iwapo Rais Kikwete hatasaini muswada huo na
kuurejesha bungeni na iwapo wabunge nao wataupitisha tena bila
kuufanyia marekebisho, Rais atalivunja Bunge.