Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeunga mkono juhudi za Umoja
wa Boda Boda Jiji la Arusha (UBOJA) za kutaka kuanza kusajili wanachama wake
pamoja na vituo vyote kwa njia ya kisasa katika mfumo wa kompyuta kama hatua ya
kuweka kumbukumbu itakayosaidia watambulike haraka kwa sura, majina yao, vyombo
vyao vya usafiri na maeneo yao wanayoishi kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya.
Akizungumzia nia ya kufanya hivyo na namna itakavyotekelezwa
jana katika ukumbi wa bwalo la Polisi ulilopo jijini hapa, Mwenyekiti wa UBOJA Bw.
Maulid Makongoro alisema kwamba wameamua kufanya hivyo ikiwa ni mkakati wa
kuliunga Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu.
Bw. Makongoro alieleza ili kufanikisha suala hilo la usajili,
kila kituo kitatakiwa kwanza kilipe ada ya mwaka mzima lakini pia kitatakiwa
kulipia gharama ya Shilingi 20,000 ambapo wanachama wake bila kujali idadi
waliyonayo wote watapigwa picha na taarifa zao zitapelekwa kwa viongozi wa
wilaya likiwemo Jeshi la Polisi lakini pia kila mmoja atakuwa na kitambulisho.
“Usajili wa awali ulikuwa wa kibubu bubu kwa mfano baaadhi ya
vituo vilikuwa vinamsajili mwanachama bila kumpiga picha lakini kumbukumbu
zilikuwa hazifiki ngazi ya juu lakini wa sasa utakuwa wa Kidijitali kwa kuwa
ofisi ya UBOJA itakuwa na kumbukumbu hizo kwenye vitabu na kwenye mfumo wa
kumbukumbu wa Kompyuta”. Alifafanua Bw. Makongoro.
Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuwadhibiti watu
wanaofanya uhalifu kwa mgongo wa waendesha boda boda jambo ambalo linaweza kuwaletea
taswira ambayo si nzuri machoni mwa watu.
Naye mgeni rasmi wa mkutano huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba, Jeshi la Polisi
linaunga mkono moja kwa moja wazo hilo la UBOJA kwani hatua hiyo itasaidia
kudhibiti uhalifu.
Alisema hatua hii inaonyesha nia njema walionao UBOJA kwa
Jeshi la Polisi katika kushirikiana na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika
jiji la Arusha lakini pia mbali ya kuonyesha taswira nzuri kwa jamii itawasaidia
kwa usalama wao.
Kamanda Mkumbo alisema kwa hivi sasa ushirikishwaji wa jamii
katika kudhibiti uhalifu ni muhimu sana na kuwataka waendelee kuliunga mkono
Jeshi hilo kwa kutoa taarifa mbalimbali za uhalifu hasa unaotokea maeneo yao ya
kazi.
“Kwa hivi sasa wezi wengi wanapenda kuwatumia kwa kuwakodi
waendesha pikipiki; kukagua eneo la kufanya uhalifu lakini pia baada ya kufanya
uhalifu wanatoroka kwa pikipiki hivyo ukimgundua mtu wa namna hiyo toa taarifa
haraka kwa askari yeyote unayemuamini au kwa viongozi ili tumkamate”. Alisisitiza
Kamanda Mkumbo.
Aliwaasa katika utendaji wao wa kazi kutoweka mbele sana pesa
bali waangalie uhai wao kwanza hasa wanapoona baadhi ya abiria wanawakodisha
kwa pesa nyingi na kuwapeleka maeneo tete hasa usiku kwani wengine hawana nia
nzuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa
Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Joseph Charles Bukombe, aliwataka wananchi wote
wa mkoa huu wafuate sheria za usalama barabarani kwani kwa kufanya hivyo hakuna
mtu atakayewakamata.
Mkuu huyo wa Usalama Barabarani alisisitiza suala la kuvaa
kofia ngumu “Helmet” kwa dereva na abiria na kusema hatakuwa na msamaha kwa mtu
yeyote atakayekaidi hilo awe mtumishi wa serikali au mwendesha pikipiki za
abiria na kuongeza kwamba endapo vyombo vya usafiri vitaendeshwa salama basi vitabaki
salama na watu watakuwa salama na kutaja kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya
nenda kwa Usalama Barabarani inayosema “ENDESHA
SALAMA HATUTAKI AJALI TII SHERIA TUNATAKA KUISHI”.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii
mkoani hapa Mrakibu Msaidizi (ASP) Edith Makweli na msaidizi wake Mkaguzi wa
Polisi Shabani Shabani ulihudhuriwa na washiriki 220 toka kanda tano ambao ni
viongozi wa kata na vituo vya waendesha pikipiki ambapo Jiji la Arusha
linakadiriwa kuwa na jumla ya vituo vya bodoa boda 400.